CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kinatarajiwa kuendelea na maandamano yake ya amani leo jijini Mwanza, ikiwa ni mwanzo wa awamu ya pili ya maandamano hayo katika majiji yote nchini.
Maandamano hayo yanafanyika licha ya taifa kuwa katika siku ya mwisho ya maombolezo ya siku tano ya kifo cha aliyekuwa Waziri Mkuu na Mgombea urais (CHADEMA) mwaka 2015, Edward Lowassa.
Akizungumza na Nipashe kuhusu maandalizi ya maandamano na mkutano na wananchi uliopangwa kufanyika kwenye viwanja vya Furahisha, Naibu Katibu Mkuu CHADEMA Tanzania Bara, Benson Kigaila, alisema maandamano hayo hayatasitishwa kutokana na msiba huo, bali msiba huo utakuwa sehemu ya kuenzi maisha ya Lowassa.
Kigaila alisema katika kutekeleza maandamano hayo, CHADEMA itakuwa inaeneza demokrasia aliyokuwa anaishi Lowassa kwa kuwa licha ya kifo chake, lazima chama kiendelee na kazi ya kutetea wananchi kupitia maandamano hayo na mkutano wa kuihimiza serikali kushusha gharama za maisha.
"Kifo cha ndugu yetu Lowassa ambaye anatambulika serikalini kama aliyewahi kuwa Waziri Mkuu wa Taifa hili, hakiwezi kutuzuia kuendelea na utetezi wa haki za Watanzania, bali tutafanya hivyo kwa kuyaenzi maisha yake na mazishi yake tutashiriki pia," alisema Kigaila.
Akithibitisha ushiriki wa viongozi wote wa chama hicho kitaifa, Katibu wa CHADEMA Kanda ya Victoria, Zakaria Obad, alisema kuwa katika maandamano hayo, aliyewahi kuwa Katibu Mkuu wa CHADEMA, Dk. Wibroad Silaa, Wakili Boniface Mwabukusi na Mwanaharakati Mdude Nyagali, maarufu Mdude CHADEMA, wanatarajiwa kuwa sehemu ya watakaoshiriki.
"Pia viongozi wote wa CHADEMA kitaifa wamethibitisha kushiriki katika maandamano na mkutano huu, hivyo niwakumbushe wafuasi na wasiokuwa wafuasi wa CHADEMA kushiriki kikamilifu maandamano haya kuishinikiza serikali kuweka mikakati ya kushusha hali ya maisha," alisema Obad.
Alisema katika maandamano hayo wanaishinikiza pia serikali kusikiliza maoni ya wananchi kuhusu miswada mitatu ya Sheria ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani pamoja na wa Sheria ya Vyama vya Siasa ambayo tayari imepitishwa na Bunge ikisubiri kutiwa saini na Rais.
Mwandishi wa habari hizi ameona nakala za barua zinazowapa rukhsa CHADEMA kuendelea na maandamano hayo kutoka ofisi za Mkuu wa Polisi Wilaya (OCD) Nyamagana na Ilemela, pia nakala ya barua toka kwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED