Cheo cha Zitto chavutia vigogo ACT - Wazalendo

By Halfani Chusi , Nipashe
Published at 10:32 AM Feb 19 2024
Makamu Mwenyekiti Bara wa ACT Wazalendo Dorothy Semu amechukua fomu ya kugombea nafasi ya Kiongozi wa Chama inayoshikiliwa na Zitto Kabwe ambaye anamaliza muda wake.
PICHA :ACT-WAZALENDO
Makamu Mwenyekiti Bara wa ACT Wazalendo Dorothy Semu amechukua fomu ya kugombea nafasi ya Kiongozi wa Chama inayoshikiliwa na Zitto Kabwe ambaye anamaliza muda wake.

JOTO la uchaguzi ndani ya Chama cha ACT - Wazalendo limeendelea kupanda. Makamu Mwenyekiti wa chama hicho Tanzania Bara, Dorothy Semu na Waziri Kivuli wa Katiba na Sheria, Mbarala Maharagande, wamechukua fomu kuwania nafasi ya Kiongozi Mkuu wa chama hicho, ambayo sasa iko chini ya Zitto Kabwe.

Nimeamua, ninaamni kwenye uongozi wa pamoja, nimekitumikia chama hiki kwa miaka minane katika nafasi mbalimbali, wakati chama kilipopita kwenye misukosuko ya kidemokrasia na mpaka kikataka kufutwa, nilisimama tulishirikiana na kuhakikisha kinapata hati safi," ametamba Dorothy Semu.

Akifungua pazia la kunadi sera zake, Dorothy, baada ya kuchukua fomu , amesema atahakikisha chama hicho kinabaki kuwa sauti kuu ya Watanzania zinapotokea changamoto mbalimbali.

Pia amesema atahakikisha chama hicho kinakuja na sera mbadala zinazotekelezeka na kujibu shida za Watanzania na kuwaunganisha wanachama wote kuwa kitu kimoja.

Amesema atasaidia kufanya viongozi wao kuwa bora na kufanya chama hicho kuwa mfano. Anataka kukifikisha chama hicho kwenye ushindi utakaoweka rekodi.

"Nimeamua, ninaamni kwenye uongozi wa pamoja, nimekitumikia chama hiki kwa miaka minane katika nafasi mbalimbali, wakati chama kilipopita kwenye misukosuko ya kidemokrasia na mpaka kikataka kufutwa, nilisimama tulishirikiana na kuhakikisha kinapata hati safi," ametamba.

Naye Maharagande amesema ataitumia nafasi hiyo katika maeneo mengi ikiwamo kusimamia malengo na madhumuni ya chama, misingi yake, falsafa na itikadi.

"Nitahakikisha kwa kushirikiana na viongozi wenzangu, kwa kutumia njia mbalimbali tunashinikiza utekelezaji makubaliano kati ya Marehemu Maalim Seif na Dk. Hussein Ali Mwinyi Rais wa Zanzibar yanatekelezeka kwa vitendo na kwa ratiba mahususi.

"Nitashughulikia masuala ya demokrasia, siasa na uchaguzi kwa ujumla wake na kuhakikisha tunaendeleza madai ya kuwa na muungano wa haki na usawa wenye maslahi kwa pande zote mbili," amesema Maharagande huku akishangiliwa na wafuasi waliokuwa wamefurika katika ofisi za makao makuu ya chama hicho, Magomeni, Dar es Salaam. 

Juzi, mwanachama Isihaka Mchinjita alichukua fomu kuwania nafasi ya Makamu Mwenyekiti wa ACT Wazalendo Taifa, huku akijinadi akishinda nafasi hiyo, atasaidia kujenga chama.

Baada ya kuchukua fomu hiyo, Mchikita alisema kilichomsukuma kuchukua fomu ni mapenzi ya dhati, anataka kupigania demokrasia pana yenye maslahi ndani ya nchi, kuimarisha ngome za chama na kuzifanya kuwa nyenzo muhimu ya kuunganisha Watanzania kupigania haki na ustawi wa taifa.

Amesema atasaidia kujenga misingi imara ya kitaasisi, kuimarisha sera na mwenendo wa chama ili kisimame kama kiongozi mwenye kusukuma na kushinikiza utekelezaji agenda zenye maslahi kwa wananchi.

"Sote tunafahamu chama chetu kimepita katika hatua kubwa ya ukuaji ndani ya muda mfupi. Hiki ndicho chama chenye umri mdogo kuliko vyote nchini. 

"Nafasi yangu ya uenyekiti wa mkoa niliyochukua Lindi nilikikuta chama hakina hata tawi moja, mpaka leo nimekiwezesha kuwa na uongozi uliokamilika kuanzia ngazi ya tawi, kata na mkoa. Hii inanipa ujasiri wa kuona ninaweza kutumikia nafasi ninayoiomba," ametamba.

Mbali na Mchinjita, watiania wengine waliojitokeza ni Husna Sungura anayegombea nafasi ya ujumbe wa Kamati Kuu kupitia Kanda ya Pwani na Halima Nabalang'anya anayegombea nafasi ya ujumbe wa Kamati Kuu kupitia Kanda ya Kusini.