ALIMANUSURA vurugu zitokee jana kwenye maandamano ya amani ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) baada ya msafara wa Makamu Mwenyekiti wa chama hicho, Tundu Lissu, kuingiliana na ule wa Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Dotto Biteko.
Sisi tumeandamana kwa lengo la kufikisha serikalini kero ambazo zinatukabili lakini Naibu Waziri Mkuu badala ya kutusikiliza, anataka kutugonga na gari. Watanzania wanachotaka ni kupunguziwa gharama za maisha,” amesema Sugu.
Vurugu hizo nusura zitokee eneo la Sae jijini Mbeya wakati waandamanaji walipokuwa katika barabara kuu ya Tanzania na Zambia (TANZAM) wakitokea Uyole kwenda kwenye uwanja ulioandaliwa kwa ajili ya mkutano wa hadhara, Ruanda Nzovwe.
Wakiwa katika maandamano huku wakiimba nyimbo za hamasa, nyuma yao ulitokea msafara wa Dk. Biteko ambaye alikuwa anatokea kwenye ziara ya kukagua miradi ya maendeleo wilayani Rungwe.
Askari waliokuwa wanaongoza msafara wa Biteko, wameamuru waandamanaji kupisha barabara ili upite kwanza hali ambayo ilizua kutoelewana baina ya pande hizo mbili.
Kutokana na hali hiyo, Lissu aliwataka wafuasi kuendelea na maandamano huku akiwataka askari waliokuwa wanaongoza msafara wa Biteko kupita njia nyingine au waendelee kufuata nyuma ya waandamanaji.
Amesema jana wao ndio waliokuwa na kibali cha kuitumia barabara hiyo na kwamba hakukuwa na taarifa zozote za kiongozi mwingine kuitumia kwa wakati huo.
“Waandamanaji naomba tuendelee na maandamano kwa mwendo ambao tumetoka nao. Gari yoyote ambayo inashiriki maandamano ije nyuma yetu lakini hatupishi mtu yeyote. Polisi ambao mnaongoza huo msafara tafuteni njia nyingine,” amesema.
Baada ya maelezo hayo, askari waliokuwa wanaongoza msafara wa Naibu Waziri Mkuu Biteko walielekeza magari ya msafara kupita kwenye barabara ya vumbi, hivyo kuruhusu waandamanaji kuendelea na safari.
Akizungumza kwenye mkutano wa hadhara, aliyekuwa Mbunge wa Mbeya Mjini kupitia CHADEMA, Joseph Mbilinyi, maarufu kama Sugu, amesema lengo la polisi waliokuwa wanaongoza msafara walitaka kuwagonga waandamanaji.
Amesema Biteko alitakiwa autumie mkutano huo wa hadhara kuwaeleza wananchi waliokuwa wamekusanyika kuhusu namna ambavyo amejipanga kutatua kero ya umeme kutokana na kukatika mara kwa mara.
Sugu amesema wananchi wamekuwa wakipata shida kwa kushindwa kufanya shughuli za maendeleo kutokana na uhaba wa umeme, hivyo akamtaka kuwaeleza wananchi ukweli.
“Sisi tumeandamana kwa lengo la kufikisha serikalini kero ambazo zinatukabili lakini Naibu Waziri Mkuu badala ya kutusikiliza, anataka kutugonga na gari. Watanzania wanachotaka ni kupunguziwa gharama za maisha,” amesema Sugu.
Viongozi, wanachama wa CHADEMA pamoja na wananchi kutoka mikoa ya Kanda ya Nyasa waliandamana kwenye misafara mitatu tofauti. Msafara wa kwanza wa maandamano ya kilomita 18, uliongozwa na Mwenyekiti wa Taifa, Freeman Mbowe, kuanzia Mbalizi, msafara wa pili ukiongozwa na Lissu ulianzia Uyole na mwingine uliokuwa unaongozwa na Katibu Mkuu, John Mnyika, ulianzia Isanga.
MVUA YAVUNJA MKUTANO
Baada ya kutamatika kwa maandamano, kulifuatia mkutano wa hadhara uliopangwa kufanyika uwanja wa Ruanda, Nzovwe, lakini ulivunjika baada ya mvua kubwa kuanza kunyesha. Mvua hiyo ilianza kunyesha saa 10:08 jioni.
Baada ya maandamano hayo kufika kwenye uwanja huo, viongozi walijipanga kwa ajili ya kuanza kuhutubia. Walianza viongozi wa dini kuomba dua na sala.
Wakati viongozi hao wakijiandaa kuhutubia, iliibuka mvua ambayo iliambatana na upepo na kusababisha wananchi kwenda kujificha kwenye makazi ya watu jirani na uwanja huo. Baada ya mvua hiyo kuzidi, viongozi walipanda magari na kuondoka uwanjani.
MABANGO
Waandamanaji walikuwa wamebeba mabango yenye ujumbe mbalimbali ambao ulikuwa unaelezea kero mbalimbali zinazowakabili ikiwamo ukali wa maisha.
Baadhi ya mabango yalikuwa na ujumbe unaosema ‘Umeme umekuwa kero, tunashindwa kufanya kazi,’ mabomba tunayo, bili ziko juu ila maji hayatoki’, ‘Kikokotoo kinatuhusu na sisi,’ ‘Tunataka Katiba Mpya,’ ‘Tunamtaka Rais asisaini miswada ya uchaguzi iliyopitishwa na bunge’.
Mabango mengine yalisema ‘Gharama za maisha ziko juu, sukari bei juu, mafuta yanapanda kila siku’ na ‘tunataka bandari yetu’.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED