CHAMA cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Morogoro, kimewataka wanaCCM kufanya uchaguzi wa serikali za mitaa kuwa wa huru na haki kuanzia kura za maoni hadi uteuzi, na kwamba pesa au utajiri wa mtu usiwe kigezo cha kupewa uongozi.
Mwenyekiti wa CCM mkoani humo, Mhandisi Joseph Masunga amesema katika chaguzi za mwaka huu 2024 chama kitahakikisha kinasimamia kwa ukaribu ili kuhakikisha michakato yote inafanyika pasipo kuhusisha rushwa.
Aidha, Masunga amesema kila mgombea anapaswa kujipanga kuchaguliwa kulingana na sifa zake za uongozi alizonazo au kukubalika kwake kwa wananchi.
Amesema masuala ya rushwa ni ya kijinai yanayopaswa kushughulikiwa kijinai ambapo mtu atakapokutwa na changamoto hiyo ikithibitika sheria kupitia mahakama zitachukuliwa huku chama kikijipanga kumshugulikia kimaadili.
Hivi karibuni Taasisi ya kuzuia na kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Morogoro ilivitaka vyama vya siasa kufanya chaguzi zao kwa kuzingatia sheria zilizopo ili kujiepusha na masuala ya rushwa.
Akizungumzia hilo Mkuu wa TAKUKURU mkoa wa Morogoro, Tungaraza Manyama, ameitaka jamii kushirikiana na serikali katika kukabiliana na masuala ya rushwa kwa kutoa taarifa za wanaotoa au kupokea rushwa kwenye chaguzi zinazotarajia kuanza mapema mwaka 2024.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED