Wanafunzi wasiozingatia kuvaa sare sahihi, lazima sheria ichukue nafasi

By Sabato Kasika , Nipashe
Published at 04:17 PM Apr 16 2024
Wanafunnzi wa shule ya sekondari.
PICHA: MAKTABA
Wanafunnzi wa shule ya sekondari.

HIVI karibuni nilifika katika shule moja ya sekondari ya serikali ndani ya Dar es Salaam, kuonana na mkuu wa shule hiyo kwa masuala binafsi.

Nikiwa ofisini mwake, nikaona ‘vipande’ vingi vya suruali. ‘Vipande’ hivyo vilikuwa chini kwenye kona ndani ya ofisi hiyo. Baada ya kumaliza kuelezea kile kilichonipeleka shuleni hapo, nilijaribu kumuuliza kuhusu vipande hivyo ni vya nini. 

Mkuu huyo wa shule akasema, vimekatwa kutoka kwenye suruali za baadhi ya wanafunzi, ambao wanashona sare kwa kukiuka maelekezo ya shule kwa kuzibana chini kama 'vimodo'.

Kwa mujibu wa mkuu huyo wa shule, kila mwanafunzi anayevaa sare hasa suruali ambayo imepunguzwa vipimo kwa chini na kuwa 'modo', inakatwa kuanzia magotini na kipande kubaki ofisini.

Inapokatwa, upande mmoja wa suruali unaishia magotini na mwingine hadi chini, hivyo inakuwa si rahisi mwanafunzi kwenda nayo shule, analazimika ashone nyingine upya kwa kuzingatia maelekezo ya shule.

Nikirejea kwenye hoja yangu ni kwamba, suala la kuzingatia na kuheshimu utaratibu wa shule ni muhimu, badala ya kila mwanafunzi kujifanyia anavyotaka kwa kushona sare kinyume.

Suala la sare linasisitizwa shuleni na linafuatiliwa kwa makini kuanzia mwonekano wa mwili hadi tabia, kwa sababu ni yote hayo ni ya muhimu kwa maendeleo ya mwanafunzi kitaaluma.

Wanafunzi wa kike wanatakiwa kusuka nywele mistari sita na siyo zaidi ya hiyo na ikiwa hawezi kusuka mistari hiyo, anatakiwa kunyoa nywele ziwe ndogo za kufaa kuchana kwa kitana kidogo.

Kwa wanafunzi wa kiume, wanatakiwa kunyoa nywele kwa mfumo unaofanana kwa maana ya unyoaji wa nywele zinazofaa kuchana kwa kitana kidogo na si vinginevyo.

Lakini cha kushangaza, baadhi ya wanafunzi wamekuwa wanaenda kinyume na utaratibu huo, ingawa wanajua wazi kuwa ni makosa  kutofuata maelekezo ya shule.

Nitoe mfano tu, ni ngumu hata kukuta hasa katika shule za serikali, wanafunzi wamechomekea mashati yao, na baadhi wamezikata inakuwa vigumu kuchomeka.

Nadhani kuna haja ya kuwapo kwa uhusiano mzuri kati ya wazazi na walimu kwenye suala la malezi, ili kudhibiti vitendo ambavyo vinafanywa na wanafunzi wachache wasiojali umuhimu wa elimu.

Wazazi wafuatilie watoto wao kwa karibu, kwani inashangaza kama wamewashonea sare, halafu watoto wanakwenda kwa mafundi kupunguza upana ili ziendane na wanavyotaka wao na si matakwa ya shule.

Katika kufanikisha hilo, wazazi, waache mtindo wa kuwafuata walimu na kuwafokea pale watoto wao wanapofanya makosa na kuadhibiwa, kwani mtindo huo unavuruga uhusiano kati ya makundi hayo mawili.

Ikumbukwe kuwa, wanavyovaa kinyume na utaratibu wa shule, ndivyo wanavyoonyesha walivyo kwamba wao ni wa aina gani, hivyo ushirikiano ungesaidia kuwanusuru kutoka katika mazingira hayo.

Imekuwa kawaida kukuta baadhi ya wanafunzi wakiwa vijiweni katika vituo vya daladala wamevaa sare hasa suruali ‘mlegezo’ na tena zimebana kwa chini, huku wamening'niza vitamba kwenye mifuko ya nyuma. Wengine huenda mbali. Viatu vyao ni jamii ya kandambili, jambo ambalo ni kosa kubwa.

Nadhani si sahihi mwanafunzi ambaye anatarajia kuwa mtaalam, kiongozi na msomi wa baadaye kuwa wa aina hiyo. Ni vyema wakasaidiwa wajitambue na kufuata kile kilichowapeleka shule na wanapokuwa wagumu, lazima utaratibu kama wa yule mkuu wa shule uchukue nafasi.

Inaelezwa na baadhi ya wanafunzi kuwa, wapo wengine katika shule hiyo niliotembelea, ambao katika suruali zao chini wameweka zipu, ili wawapo shule ziwe zinaonekana jinsi taratibu zilivyo.

Lakini, wakishatoka shule tu kila mmoja anavuta zipu, suruali inabana tena chini kama kawaida. Hivyo ingekuwa ni vyema kama hao nao watafuatiliwa ili kuwabaini na kuwachukulia hatua.

Ninajua kuna suala la utandawazi na ugumu wa maisha ambao unafanya wazazi wawe na muda mdogo kufuatilia tabia za watoto wao, lakini kwa hali ya sasa, ipo haja ya kuwafuatilia kwa karibu.

Vilevile, jamii nzima isisahau mila, utamaduni na maadili ili kunusuru kizazi hiki ambacho sasa kila mmoja anaonekana ana maamuzi yake bila kujali kwamba ni kinyume.