Waamuzi wachezeshe kwa haki kuelekea kumaliza msimu wa ligi

By Mhariri Mtendaji , Nipashe
Published at 03:35 PM May 06 2024
Waamuzi wachezeshe kwa haki kuelekea kumaliza msimu wa ligi.
PICHA: MAKTABA
Waamuzi wachezeshe kwa haki kuelekea kumaliza msimu wa ligi.

WAKATI Ligi Kuu Bara ikiwa imebakisha raundi tano tu kutamatika, bado kuna uchezeshaji usioridhisha kwa baadhi ya waamuzi. Kwa bahati mbaya sana uchezeshaji huo unaangukia kwa timu zinazosaka ubingwa, huku zile zinazotafuta nafasi ya nne ili zicheze mechi za kimataifa mwakani, au zinazokimbia kushuka daraja, zikionekana kukandamizwa zaidi.

Kumekuwa na baadhi ya matukio yanaonekana kujirudia kwa waamuzi, wakizinufaisha timu zingine na kuziumiza zingine, ambapo baadaye mamlaka husika inakuja kugundua kuwa ni makosa.

Mfano, katika mechi ya Aprili 27, mwaka huu kati ya Yanga na Coastal Union, uliochezwa, Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam, mchezaji Lameck Lawi wa Coastal Union alionyeshwa kadi nyekundu kwa kile kilichoelezwa kumvuta jezi Stephane Aziz Ki.

Hata hivyo, Kamati ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi ya Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB), ilipokea taarifa za uchambuzi wa kitaalamu kutoka kwa wakufunzi wa waamuzi, ambazo zimeainisha kuwa mchezaji huyo hakustahili kuonywa kwa kadi nyekundu, badala yake ilipaswa aonyeshwe kadi ya njano kwa sababu wakati tukio linatokea kulikuwa na mlinzi mwingine wa Coastal Union mbele yake ambaye angeweza kuufikia mpira.

Mwamuzi Rafael Ikambi aliyemwonyesha mchezaji huyo kadi nyekundu na msaidizi wake namba mbili, wakapewa onyo kali. Wakati akionyeshwa kadi timu hizo zilikuwa suluhu, lakini baada ya hapo Yanga ilipata bao 1-0.

Katika mechi ya mzunguko wa kwanza kati ya timu hizo mbili, iliyochezwa Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga, mwamuzi Emmanuel Mwandimbwa, pia alimtoa nje kwa kadi nyekundu mchezaji Semfuko Charles, Yanga ikishinda bao 1-0, lakini Kamati pia iliifuta kadi hiyo baada ya kujiridhihirisha kuwa haikustahili. Mwamuzi huyo alifungiwa miezi sita.

Februari mwaka huu, Bodi ya Ligi ilimfutia adhabu mchezaji wa Prisons, Zabona Mayombya, alipoonyeshwa kadi nyekundu na mwamuzi Ahmed Arajiga katika mechi ambayo timu hiyo ilicheza na Yanga, Februari 11.

Hatutaki kusema kwa nini mechi zote ambazo wachezaji wanaoonyesha kadi nyekundu na waamuzi na baadaye zinafutwa ni za Yanga, kwa sababu mchezaji anapofanya madhambi ni lazima aadhibiwe, lakini tunajiuliza kwa nini huwa zinafutwa baadaye? Ina maana waamuzi wanatoa kadi kwa mihemko. 

Kwa nini huwa hawajiridhishi kwanza? Kwa nini mara nyingi zinazoumizwa ni timu ndogo? Kwa nini waamuzi huwa hawakosei kuwatoa kwa kadi nyekundu wachezaji wa timu kubwa halafu baadaye zikafutwa?

Hii inaonyesha kabisa hizi timu kubwa pamoja na kuwa na wachezaji bora, wenye uwezo mkubwa, wanalipwa mamilioni ya pesa, lakini wakati mwingine timu zao zinashinda kwa msaada wa waamuzi, huku timu zinazoitwa au kujiita ndogo zikizidi kuonewa.

Hata wakiadhibiwa waamuzi kwa makosa, lakini timu hizo zinakuwa zimeshaathirika kwa kupoteza pointi ambazo wakati mwingine zitakuja kuwahukumu mwishoni mwa ligi.

Hivyo, rai yetu ni kuelekea msimu ujao, Bodi ya Ligi itunge kanuni ya kutoa adhabu kali zaidi kwa waamuzi hususan kuwasimamisha kwa msimu mzima wanaotoa adhabu kama hizo bila kujidhihirisha pasipo shaka.

Mara nyingi, watoa haki, mahakimu, au waamuzi wanaambiwa wanapotoa adhabu, hasa zile zinazokuwa na athari za moja kwa moja, wanatakiwa wajidhihirishe pasipo shaka, na iwapo kuna shaka, basi wasifanye hivyo. Ni bora kumuachia mtuhumiwa huru, kuliko kumfunga mtu asiye na hatia.

Waamuzi nao wanatakiwa kuzingatia kuwa ni bora kutotoa kadi nyekundu kama hana uhakika, kuliko kumtoa mchezaji nje wakati hastahili. Huu ni uonevu mkubwa na haupaswi kufumbiwa macho.

Tunapoelekea mwishoni kumalizia mechi za ligi, tunatamani kuona waamuzi wakiongeza umakini zaidi, ili kutompa mtu ubingwa usiostahili, au kuishusha timu daraja ambayo haikutakiwa kwenda Ligi ya Championship, ila kwa sababu ya uamuzi wao tu wa mihemko.