Uelimishaji, uhamasishaji ni muhimu matumizi nishati safi

Nipashe
Published at 09:49 AM May 10 2024
Waziri wa Nishati, Dotto Biteko.
Picha: Maktaba
Waziri wa Nishati, Dotto Biteko.

JUKUMU kubwa linalomkabili kila mwananchi hivi sasa ni umuhimu wa uelewa wa matumizi ya nishati safi katika jitihada za kupambana na uharibifu wa mazingira.

Katika hili kuna kila sababu ya kuongeza uelewa wa wananchi na taasisi kuhusu umuhimu wa matumizi ya nishati safi ya kupikia kupitia programu mbalimbali za uelimishaji na uhamasishaji ili kuondoa fikra hasi zinazosababisha ukinzani kwa matumizi ya nishati hizo.

Ili kufanikiwa katika utekelezaji wa matumizi ya nishati hiyo ipo haja ya kufanyika kwa mijadala ya kitaifa, majukwaa yenye ushawishi, pamoja na elimu kuanzia ngazi ya chini ya kijamii.

Linapokuja suala la matumizi ya nishati safi ni lazima pia kuwapo na maandalizi ya kumwezesha mwananchi kuwa na vifaa vitakavyomwezesha kuvipata kwa gharama nafuu na kwa urahisi ili asiweze kushawishika kubaki kwenye matumizi ya kuni na mkaa ambayo ataona ni rahisi kwake na kuendelea kuharibu mazingira.

Vifaa hivyo ni pamoja na majiko sanifu ya kupikia kwa kupunguza tozo na kodi zinazotozwa katika nishati, kutoa ruzuku na kubuni mifumo ya kifedha na teknolojia ya kuwezesha watumiaji kumudu gharama za nishati hiyo kwa kuzingatia kipato chao.

Vilevile, kuoanisha na kuhuisha sera, sheria, kanuni na miongozo wezeshi itakayofanikisha matumizi ya nishati safi ya kupikia kwa kuandaa miongozo ya viwango vya ubora wa nishati, vifaa na majiko ya kupikia, kuweka mifumo na kanuni za usimamizi wa mnyororo wa thamani wa nishati safi ya kupikia, pamoja na kujumuisha masuala ya nishati safi ya kupikia katika mipango ya matumizi ya ardhi na ujenzi wa majengo ya makazi na biashara.

Kuhamasisha uwekezaji katika nishati safi ya kupikia kwa kuweka mazingira wezeshi kwa sekta binafsi kutumia fursa za biashara zilizopo katika mnyororo wa thamani wa nishati safi ya kupikia, na kuhamasisha matumizi ya mifuko ya fedha na programu za kitaifa katika kukuza na kuendeleza uwekezaji nchini. Jitihada hizi zinajumuisha uandaaji wa kanzidata ya takwimu na taarifa kuhusu nishati safi ya kupikia, mikopo yenye riba nafuu na kuhamasisha biashara ya kaboni katika miradi ya nishati safi ya kupikia.

Katika kuhakikisha kuwa jambo hili linafanikiwa ni muhimu kuwajengea uwezo watekelezaji wa miradi ya nishati safi ya kupikia kwa kutoa elimu ya ufundi na mafunzo stadi kuhusu nishati hiyo na kutoa elimu na kufunga miundombinu ya kupima viwango vya ubora wa nishati, vifaa na majiko ya nishati safi ya kupikia, mafunzo kwa wajasiriamali kuhusu matumizi yake na kuzingatia ushiriki wa wazawa katika miradi yake.

Vilevile, kujumuisha masuala ya nishati safi katika mitaala ya kufundishia shuleni ili kujenga kizazi chenye uelewa. Aidha, utendaji kazi wa idara ya usimamizi wa biashara ya kaboni uimarishwe kupitia mafunzo ili kuongeza wigo wa utafiti na ubunifu wa teknolojia zinazohusu nishati ya kupikia kwa kuimarisha ushirikiano kati ya wawekezaji wa nishati safi ya kupikia na taasisi za utafiti na maendeleo pamoja na kutoa mafunzo kwa wakufunzi.

Pia, kutenga bajeti katika uendelezaji wa utafiti, ubunifu na uvumbuzi wa teknolojia zinazohusu nishati safi ya kupikia, kujumuisha masuala ya usawa wa kijinsia kwa kuhamasisha ushiriki wa wanawake na vijana katika mnyororo wa thamani wa nishati hiyo.