Neema kwa kinamama wanaojifungua watoto njiti

By Mhariri Mtendaji , Nipashe
Published at 12:23 PM May 02 2024
Watoto njiti.
PICHA: MAKTABA
Watoto njiti.

KATIKA maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani iliyoadhimishwa jana, serikali imetangaza kuwa kinamama wanaojifungua watoto njiti likizo yao inaanzia pale watoto watakapokuwa wametimiza miezi tisa ya kuzaliwa.

Hapo mwanzo mama akienda kujifungua ilikuwa haijalishi kama mtoto huyo amezaliwa kwa wakati au kabla na likizo yake ya kujifungua ilikuwa ikihesabika miezi mitatu kama Sheria ya Kazi inavyosema.

Kwa kuzingatia kauli hiyo ni kuwa kinamama waliokuwa wakijifungua watoto njiti walikuwa wakipunjika muda wao wa likizo kwa kuwa mtoto ambaye alikuwa amezaliwa kabla ya wakati kwa mfano amezaliwa miezi miwili kabla, mama huyo ilimbidi arudi kazini baada ya miezi mitatu wakati mtoto huyo ndio alitakiwa kupokewa duniani.

Kinamama wengi walikuwa wakipitia wakati mgumu, kwa kuwa ilikuwa ikiwalazimu kutoka kazini mapema ili kwenda kuwahudumia watoto wao.

Kila mtu anafahamu malezi ya watoto njiti yalivyo magumu kutokana na kuhitaji uangalizi wa hali ya juu na wengine mama hulazimika kumlea kwa kuwa naye kifuani muda wote ili kupata joto la mama badala ya kuwekwa kwenye mashine ya kuwasaidia kupata joto.

Wanawake wengine iliwalazimu kuacha kazi kwa sababu ya kukosa wasaidizi nyumbani wa kumsaidia kumwangalia na kumpa matunzo mazuri mtoto huyo.

Kwa hili la likizo ya kinamama wanaojifungua njiti kuongezwa limeleta tumaini kubwa kwa wanawake wengi.

Baadhi walikuwa wanaona kama kujifungua mtoto njiti ndio mwisho wao wa kufanya kazi kutokana na jukumu la kumlea mtoto huyo.

Wengi walikuwa wanakosa haki zao za msingi za kufanyakazi kwa ajili ya kupata kipato cha kutunza familia kwa kusaidiana na mwenza wake.

Kwa wale ambao walijifungua watoto hao wakiwa hawana ndoa, walipitia wakati mgumu zaidi kutokana na wenzao kuwakimbia kwa kuogopa matunzo na kuwaachia mzigo kinamama.

Mwezi Machi mwaka huu, Chama cha Wafanyakazi wa Serikali na Afya Tanzania (TUGHE), kiliomba serikali kufanya mabadiliko katika sheria zake, ili kuwaongezea muda wa siku za likizo ya uzazi wafanyakazi wanaojifungua watoto njiti.

Makamu wa Rais, Dk. Philip Mpango, akizungumza jana katika Maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi (Mei Mosi) yaliyofanyika jijini Arusha, alisema likizo ya uzazi ni miongoni mwa haki za mfanyakazi ambazo hutolewa kwa siku 84 endapo mfanyakazi atajifungua mtoto mmoja au siku 100 endapo atajifungua zaidi ya mmoja.

“Iwapo mfanyakazi atajifungua mtoto au watoto kabla ya muda wake (njiti). Mtoto au watoto husika huwekwa kwenye chumba na mashine maalum chini ya uangalizi wa madaktari na wahudumu wengine wa afya hadi pale wataalam hao watakapojiridhisha afya ya mtoto au watoto hao imeimarika,” alifafanua.

Dk. Mpango alisema iwapo mfanyakazi atajifungua mtoto au watoto njiti kupindi cha uangalizi maalum hakitahesabiwa kama likizo ya uzazi.

Hizi ni habari njema kwa kinamama na kwakweli watoto wanahitaji malezi makubwa kutoka kwa wazazi wao kwani muda huo ndio humuunganisha mama na mtoto zaidi na kutengeneza upendo.

Hivi kipindi hicho ni muhimu kwa kinamama wote na wanastahili kupata likizo hiyo.