Kilio cha wafanyakazi kuhusu kikokotoo kipatiwe ufumbuzi

Nipashe
Published at 11:12 AM May 01 2024
Rais wa Shirikisho la Wafanyakazi Tanzania (TUCTA), Tumaini Nyamhokya
PICHA: MAKTABA
Rais wa Shirikisho la Wafanyakazi Tanzania (TUCTA), Tumaini Nyamhokya

LEO ni Siku ya Wafanyakazi Duniani, maarufu kama Mei Mosi. Wafanyakazi duniani kote wanasherehekea siku hii ikiwa ni sehemu ya kumbukumbu ya wenzao waliouawa miaka ya 1880 walipoandamana kudai haki na maslahi bora pamoja na saa za kufanya kazi.

Wafanyakazi hao walikuwa wakitaka saa za kufanya kazi zipunguzwe kutoka 12 hadi nane kwa siku pia kuwapo saa moja kati ya hizo kwa ajili ya mapumziko na chakula na malipo ya saa za ziada. Sambamba na hayo, walitaka pia kuwapo kwa likizo ya mwezi kila mwaka ili kumpa mfanyakazi muda wa kupumzika baada ya kufanya kazi takriban mwaka mzima. 

Katika kuadhimisha sikukuu hii, wafanyakazi wa taasisi mbalimbali, za umma na za binafsi, hukusanyika katika maeneo mbalimbali huku wakionyesha bidhaa au shughuli wanazofanya huku wakiwa na mabango yenye ujumbe mbalimbali ambayo pamoja na mambo mengine, husisitiza tija na ufanisi mahali pa kazi, na maslahi bora.

Watanzania katika kuadhimisha siku hii ambayo kitaifa inafanyika Arusha, mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Rais Samia Suluhu Hassan. Kaulimbiu ya maadhimisho hayo kwa mwaka huu ni “Nyongeza ya Mishahara ni Msingi wa Mafao Bora na Kinga Dhidi ya Hali Ngumu ya Maisha”. 

Kaulimbiu hii inasadifu na hali ya sasa ya maisha ya wafanyakazi wengi, hasa serikalini, ambao kilio chao kikubwa ni kutoongezwa mishahara kwa miaka kadhaa pamoja na malalamiko ya kikokotoo cha mafao ya wastaafu kwamba kinawaumiza wengi na kwamba hata baada ya kustaafu wanakuwa katika maisha magumu. Kutokana na hali hiyo, ni wazi kwamba serikali ambayo siku zote imekuwa ikisema ni sikivu, itatoa kauli kuhusu jambo hilo na kuwafanya wafanyakazi wengi kuwa na kicheko. 

Suala la kikokotoo limepigiwa kelele tangu yalipofanyika mabadiliko mwaka 2018 kwamba mfanyakazi anapostaafu achukue malipo ya mkupuo asilimia 25 na kiasi kilichobaki achukue kidogo kidogo kwa muda wa miaka 12.5. Baada ya vuta nikuvute ya takriban mwaka, serikali chini ya aliyekuwa Rais John Magufuli, ilisimamisha hadi mwaka 2023 na kutaka majadiliano yafanyike ili kuwapo na maelewano baina ya wafanyakazi kupitia vyama vya wafanyakazi na serikali yenyewe. 

Hatimaye mwaka jana yalifanyika tena mabadiliko na kuamuliwa kwamba malipo ya mkupuo yawe asilimia 33 kwa wafanyakazi wote wa serikali na sekta binafsi jambo ambalo limekuwa ikilalamikiwa pia kwamba kiwango hicho badi ni matesi kwa mtumishi. Swali linalokuja ni kwamba iweje mfanyakazi huyo ambaye ametumika kwa uaminifu na kupoteza nguvu zake katika ajira apewe kiasi kidogo huku kukiwa na msemo wenye mzaha kwamba akipewa kiasi kikubwa atatumia ovyo na hatimaye ataishiwa, hivyo kuwa kuishi kwa taabu katika miaka iliyobaki. 

Ili kufikia mwafaka, kwa mujibu wa Rais wa Shirikisho la Wafanyakazi Tanzania (TUCTA), Tumaini Nyamhokya, kikokotoo kibadilishwe na kutoka asilimia 33 ya sasa hadi 50 kwa malipo ya mkupuo na kanuni ya ukokotoaji iwe 1/540 kama ilivyokuwa zamani badala ya 1/580 ya sasa. 

Jambo hilo pia limezungumzwa kwa kina na baadhi ya wabunge na viongozi wa vyama vya siasa kwamba mfanyakazi huyo ambaye amefanya kazi kwa nguvu zote na hatimaye kufikia umri wa kustaafu, ni vyema apewe stahili yake ili afurahie jasho lake alilolitoa katika utumishi badala ya kubanwa na kukejeliwa kwamba hana uwezo wa kutunza fedha zake, hivyo apewe kiasi na kinachobaki atachukua kidogo kidogo. 

Aidha, katika mfumo huo wa mafao, inabainishwa kwamba iwapo mfanyakazi huyo atafariki kabla ya miaka 12.5 ya kuchukua kidogo kidogo, basi wategemezi wake watapokea mafao hayo kwa miaka mitatu pekee! 

Katika suala hili, ni vyema kukafikiwa mwafaka kama Rais Samia anavyotaka mambo yaendeshwe kwa 4R ikiwamo ‘Reconciliation’ (maridhiano) ambayo ni msingi bora katika kukubaliana kwenye jambo lolote badala ya kuacha upande mmoja ukinung’unika.