Minara ya simu kwenye makazi ya watu haina madhara

Nipashe
Published at 02:49 PM Apr 30 2024
Minara ya simu kwenye makazi ya watu.
PICHA: MAKTABA
Minara ya simu kwenye makazi ya watu.

KWA muda mrefu kumekuwa na hofu katika jamii kutokana na dhana ya kuamini kuwa kujengwa kwa minara ya simu kwenye makazi ya watu kunaathiri afya zao na hata kusababisha saratani.

Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Nguvu za Atomu Tanzania (TAEC), Profesa Lazaro Busagala, akizungumza katika kikao kazi na waandishi na wahariri wa vyombo vya habari nchini, ameondoa hofu hiyo kwa wananchi.

Wataalamu wanaeleza kuwa mtu anaweza kukaa chini ya mnara wa simu mionzi yake isimpate.

Tabia ya mionzi inaenda wima na inapiga juu na sio chini kama inavyodhaniwa na mtu asidhurike.

Tume ya Mionzi inafafanua kuwa hakuna taarifa za mionzi kutoka kwenye minara ya simu za kuwapo madhara kwa binadamu nchini kutokana na minara hiyo.

Dhana hiyo potofu inayoendelea kujengeka kwenye jamii nchini kuwa minara hiyo ina madhara makubwa kiafya kutokana na mionzi yake kusambaa kwenye makazi ya watu sasa inaondolewa na tume hiyo.

Minara ya simu ilianza kusimikwa sehemu mbalimbali nchini baada ya kuongezeka kwa matumizi ya simu za mikononi na kuzua mkanganyiko na mgawanyiko katika jamii kutokana na baadhi ya watu kujitokeza kupinga ujenzi wake.

Kauli hiyo ya Profesa Busagala imeondoa dhana hiyo potofu na jamii inapaswa kuamini minara hiyo ya simu inajengwa kwa ajili ya maendeleo yao na taifa.

Vile vile, kurahisishia wananchi kupata mawasiliano ya simu kila teknolojia inapoendelea kukua.

Jamii inapaswa kutambua kuwa zama zile, kulikuwa na tatizo kubwa la ukosefu wa mawasiliano kwenye baadhi ya maeneo kutokana na ukosefu wa minara ya simu.

Hivyo kila siku zinavyosonga mbele, teknolojia ya mawasiliano ya simu za mkononi inavyokua, jamii inapaswa kuondokana na dhana hizo potofu na kuunga mkono jitihada za serikali zinazolenga kuwaletea maendeleo, kuboresha maisha na kuinua kiwango chao cha uchumi.

Mawasiliano ya simu nchini yanavyozidi kukua yamefungua fursa ya biashara kupitia simu za mkononi na kurahisisha usafirishaji wa bidhaa mbalimbali ikiwamo za mazao ya wakulima kutoka mashambani hadi mjini.

Lengo la tume hiyo ni kuhakikisha kuna usimamizi, udhibiti na uhamasishaji wa matumizi ya amani na salama ya teknolojia nyuklia nchini.

Ifahamike kuwa tume hiyo inadhibiti madhara ya mionzi kwa kupima kiwango cha mionzi kwenye minara ya simu na rada za mawasiliano.

Pia inafanyakazi ya kudhibiti usalama wa mnyororo wa vyakula kwa kupima sampuli za vyakula, mbolea, vyakula vya wanyama, tumbaku na mazao ikiwa pamoja na vinavyoingizwa na kutoka nchini.

Kazi nyingine ni kupima sampuli za mazingira ili kubaini uchafuzi wa mionzi kwenye mazingira hivyo kudhibiti madhara ya mionzi kwa kutoa huduma ya upimaji kwa wafanyakazi wanaofanyakazi kwenye maeneo yenye vifaa vya mionzi kukusanya, kusafirisha na kuhifadhi mabaki ya vyanzo vya mionzi ili kuepuka kuhatarisha maisha ya wananchi.

Huduma za matengenezo ya vifaa vinavyotumia teknolojia ya nyuklia hospitalini kama vile X- Ray, CT-Scan, MRI na kwa upande wa sekta za ujenzi, kilimo, viwanda na kuratibu miradi inayotumia teknolojia ya nyuklia nchini.