SHAMBULIO LA LISSU: Familia yake yadai haki kwa AG

By Elizabeth Zaya ,, Jenifer Gilla , Nipashe
Published at 09:18 AM May 21 2024
Kaka wa Lissu, Alute Lissu, (kushoto) akizungumza jana jijini kwao jimboni Singida Mashariki, (kushoto) Makamu Mwenyekiti  wa CHADEMA Tanzania Bara, Tundu Lissu.
Picha: Mpigapicha Wetu
Kaka wa Lissu, Alute Lissu, (kushoto) akizungumza jana jijini kwao jimboni Singida Mashariki, (kushoto) Makamu Mwenyekiti wa CHADEMA Tanzania Bara, Tundu Lissu.

NGUO zenye damu ya Tundu Lissu pamoja na gari lake lenye matundu ya risasi vinapelekwa Makumbusho ya Taifa, familia ya Makamu Mwenyekiti huyo wa CHADEMA Tanzania Bara sasa inataka haki kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG).

Ijumaa iliyopita, Jeshi la Polisi Mkoa wa Dodoma lilimkabidhi Lissu gari lake aina ya Toyota Landcsruiser V8, VXR lililolishikilia tangu Septemba 7, 2017 aliposhambuliwa kwa risasi akiwa ndani ya gari hilo. 

Kukiwa na mpango huo wa kulihamishia Makumbusho ya Taifa gari hilo, familia ya Lissu inaona hatua ya polisi kukabidhi gari hilo haitoshi; inataka vyombo vya sheria vitimize wajibu wake kwa kuwasaka na kuwatia hatiani waliohusika na shambulio hilo. 

Kaka wa Lissu, Alute Lissu, akizungumza kwa niaba ya ndugu zake jana jijini kwao jimboni Singida Mashariki, alisema wao kama familia pamoja na Watanzania wengine, wanataka haki itendeke na hawatachoka kutafuta haki hiyo. 

Ni kauli ya familia yao iliyotolewa baada ya Lissu kwenda kijijini kwao kuonesha gari hilo ikiwa ni siku chache baada ya kukabidhiwa na Jeshi la Polisi. 

"Sisi kama ukoo bado tunalia kwamba haki itendeke, kuhakikisha wale watu waliotaka kuchukua maisha ya Lissu kabla ya muda wake, wasakwe na kupelekwa mbele ya sheria ili waadhibiwe kwa sababu wamefanya jambo la uovu kabisa. 

"Kwa hiyo, tutaendela kusisitiza na kutaka kufahamu na ninafikiri siyo sisi peke yetu, ni pamoja Watanzania. Kwa ujumla wao wanatamani kujua ni nini na nani waliotaka kuondoa uhai wa huyu ndugu yetu. 

"Mtanzania huyu ambaye ni sawa na Mtanzania yeyote, ana haki ya kuishi au kufa uzeeni, ana haki ya kupakata wajukuu zake, si kukatishwa maisha katikati halafu lisitokee jambo lolote," alisema. 

Alute alisema ni lazima kuwe na uwajibikaji wa vyombo vyenye jukumu hilo kujua kitu gani kilitokea, kwa sababu gani na hatua iliyofikiwa katika upelelezi wa polisi kwa waliotaka kumuua. Alisisitiza wanayo haki ya kufahamu hilo. 

Kaka huyo wa Lissu alieleza kuwa mdogo wake aposhambuliwa na kupelekwa Nairobi, Kenya kwa ajili ya matibabu ya kibingwa, alifuatilia kutafuta haki ikiwamo kwa Jeshi la Polisi na kutaka kufanyike uchunguzi wa kina, hali kadhalika kwa AG kuwasilisha hoja hiyo hiyo. 

"Labda niseme kwamba ndugu yangu huyu alipopatwa na shambulio na kupelekwa Nairobi kwa ajili ya matibabu, mimi na ndugu zangu tulikuwa tunafuatilia mambo yake na kumsemea na katika kumsemea tulikuwa tunataka polisi wafanye uchunguzi wa kina ili kufahamu wahalifu ni kina nani na wamechukuliwa hatua gani. 

"Tulichukua hatua mpaka kuandika barua kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali na baada ya kusubiri mwezi mmoja, hatukuona kitu chochote, tulimwomba AG aombe nchi za kirafiki walete mpelelezi kutoka huko ili aje afanye upelelezi huru.  

"Hatuwezi kuchoka kudai haki hii na kesi za jinai hazina ukomo. Tuna haki na Watanzania wana haki ya kujua kilichotokea ili waovu wasitawale, maana tukikaa kimya tukiwa waoga ndivyo waovu wanatawala na hatuwezi kukubali waovu watawale kwa kweli," alisema.

 Alieleza kuwa wao familia wanataka gari alilokuwamo ndugu yao wakati anashambuliwa pamoja na nguo zake alizokuwa amevaa wakati wa tukio, vitumike kama kumbukumbu. 

"(Familia) tunafikiria kuwa pamoja na kwamba fedha hatuna, lakini (Lissu) angalie uwezekano wa kutafuta gari lingine, hili libaki kama kumbukumbu ya Septemba 7, mwaka 2017 aliposhambuliwa. 

"Kwa hiyo, tunaomba ulitunze, nguo iliyokuwa na damu siku umepigwa risasi na viatu utunze, usitupe wala usifue, kuonesha kwamba waovu hawashindi, wanaweza kushinda kwa muda mfupi lakini uovu haulipi," alitamka akimtazama Lissu. 

Alisema familia yao inamuunga mkono Lissu katika harakati zake za kisiasa, akisisitiza kwa kauli: "Hata kama anatumia lugha ya ukakasi ambayo wengine hawapendi, labda inafika wakati ambao anasema liwalo na liwe, hatuwezi kuvumilia watu wengine watuchezee."

 Katika hatua nyingine, michango ya fedha kwa ajili ya kumnunulia gari Lissu ulikuwa umefikia Sh. milioni 15.3 hadi jana mchana. 

Lissu alithibitisha kufikia kiasi hicho cha fedha ndani ya siku mbili kupitia mtandao wake wa X na kuhamasisha wafuasi wake waendelee kumchangia ili lipatikane gari la kumsaidia katika harakati zake za kisiasa. 

"Gari hili litawekwa kwenye Makumbusho kama mlivyoshauri. Gari mbadala linahitajika ili harakati za ukombozi ziendelee. Lengo ni kupata gari ndani ya mwezi mmoja. Ndani ya siku mbili, michango yenu imeshafikia Sh. 15,360,059. Kwa ukarimu wenu inawezekana," aliandika Lissu kwenye ukurasa wake huo.

Mwanaharaki Maria Sarungi anayeendesha harambee hiyo pia alithibitisha kufikiwa kiwango hicho cha fedha na kuhamasisha watu kuendelea kuchangia ili kufikia lengo ambalo halijatajwa, hata hivyo.

Katika shambulio hilo Lissu alirushiwa zaidi ya risasi 30. Kati yake, 16 zilimpata sehemu mbalimbali za mwili wake. Alipelekwa Hospitali ya Rufani ya Mkoa wa Dodoma kisha kuhamishiwa Hospitali ya Nairobi, Kenya na baadaye alipelekwa Ubelgiji kwa matibabu zaidi.