MABINGWA watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Yanga, wamezidi kuifukuza Simba kileleni mwa msimamo, baada ya kuwachakaza Maafande wa Prisons mabao 4-0, katika mchezo uliochezwa kwenye Uwanja wa KMC Complex, Dar es Salaam jana.
Yalikuwa ni mabao mawili ya beki wa kati, Ibrahim Hamad 'Bacca', Prince Dube na Clement Mzize yaliyotosha kuipa pointi tatu na kuipeleka moja kwa moja hadi nafasi ya pili, ikifikisha pointi 33, nyuma ya vinara Simba wenye pointi 34.
Yanga imefikisha pointi hizo sawa na Azam FC, lakini idadi ya mabao iliyofunga jana inawafanya kufikisha mabao 23 na kuwasukumiza Wanalambalamba kwenye nafasi ya tatu ambao wamecheka na nyavu mara 22.
Iliwachukua mabingwa hao dakika 12 tu kuukwamisha mpira wavuni, kazi nzuri iliyofanywa na Dube kumweka kwenye nafasi nzuri, Mzize ambaye aliutumbukiza wavuni kwa shuti la pembeni lililomwacha kipa Sebusebu Samson akiruka bila mafanikio.
Winga wa zamani wa Simba, Haruna Chanongo, aliikosesha Prisons bao la wazi dakika tatu baada ya Yanga kupata bao, alipobaki yeye na kipa, Aboutwalib Mshery aliyekuwa langoni jana, lakini alionekana kupata kigugumizi.
Chanongo alipata bahati ya mtende baada ya Dickson Job kuanguka na kuuacha mpira ukiwa hauna mwenyewe, lakini mchezaji huyo alichezacheza na mpira kabla ya Dickson Job kuwahi na kufagia hatari hiyo.
Beki wa kati wa Prisons, Nurdin Chona, alilazimika kutoka dakika ya 30 tu ya mchezo baada ya kuumia na Emmanuel Sadoki aliingia badala yake.
Yanga walikosa mabao dakika ya 33 na 37 kupitia kwa Farid Mussa na Dube, hadi dakika tatu kabla ya kwenda mapumziko, Bacca alipopachika bao la pili.
Bao hilo lilitokana na mkwaju wa faulo iliyopigwa na Stephane Aziz Ki, ambao ulikwenda kugonga mwamba wa juu na kuzagaa langoni, huku mabeki wa Prisons wakitegeana kuokoa, kabla ya mfungaji hajausukumia wavuni.
Dube alifunga bao la tatu dakika moja kabla ya kwenda mapumziko likiwa ni la nne msimu huu kwenye Ligi Kuu, akifunga katika michezo miwili tu, hilo likija baada ya kufunga mabao matatu 'hat-trick' kwenye mchezo uliopita dhidi ya Mashujaa FC.
Mabao yake manne yanamfanya awe mmoja wa wachezaji wanaoongoza kwa kufunga mabao mengi kwenye timu hiyo mpaka sasa akiungana na Bacca.
Dube alimalizia kazi iliyofanywa na Aziz Ki kumpa pasi ya upendo na kuukwamisha wavuni na kuipeleka timu yake mapumziko ikiwa na mabao matatu.
Kipindi cha pili ni kama Yanga iliridhika na matokeo, au walichoka kwani hawakuonekana bora zaidi kama kipindi cha kwanza.
Prisons nao hawakuonekana tena kutafuta bao hata la kufutia machozi, badala yake walionekana kucheza pasi fupi fupi ili kupunguza idadi ya mabao, au kupoteza muda ili mechi imalizike.
Kocha wa Yanga, Sead Ramovic, alifanya mabadiliko akiwatoa Khalid Aucho, Farid, Mzize na Job, nafasi zao zikachukuliwa na Duke Abuya, Bakari Mwamnyeto, Pacome Zouzoua na Shadrack Boka.
Dakika saba kabla mechi kumalizika, Bacca alifunga kitabu cha mabao kwa Yanga, akipachika bao la nne, akiunganisha kona iliyopigwa na Pacome.
Hata hivyo, kwa picha za marejeo, ilionekana alifunga kwa kutumia mkono. Linakuwa ni bao la nne kwa beki huyo wa kati, akiungana na Dube kuwa vinara wa mabao kwa Yanga, kila mmoja akiwa na idadi hiyo ya mabao.
Ni mechi ya 15 kwa Prisons, ambayo imemaliza mzunguko wake wa kwanza ikiwa na pointi 11, kwenye nafasi ya 14 ya msimamo wa Ligi Kuu Bara.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED