Yanga yaanzia 'Gym' ikimtangaza Andambwile

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 07:54 AM Jul 10 2024
news
Picha: Yanga
Prince Dube akijifua akiwa na klabu yake hiyo mpya.

KIKOSI cha Yanga jana kimeanza rasmi maandalizi ya mashindano msimu ujao, huku klabu hiyo ikitamba kutwaa taji la kwanza nchini Afrika Kusini kwenye michuano ya Kombe la Toyota.

Ofisa Habari wa Klabu hiyo, Ali Kamwe, amesema wachezaji wapya na wa zamani waliosajiliwa wameshaanza kuwasili na itachukua muda wa siku tatu kukamilisha idadi ya wote waliosajiliwa kwa msimu ujao.

Amesema kwa siku ya kwanza wale waliowasili walipimwa afya na kuanza mazoezi ya kujenga miili yao na kuwa na pumzi zoezi ambalo litaendelea kwa wachezaji wote watakaowasili.

"Tulianza asubuhi kucheki afya zao na baadaye mazoezi ya fiziki yaliyofanyika kwenye 'gym' pale Gymkhana, Kocha Mkuu Miguel Gamondi na benchi lake la ufundi wote wameshaingia, wachezaji wengi wameshaingia, wapya na wa zamani, wote wanaonekana kuwa na furaha, hii inaleta picha kuwa tutakuwa na msimu mwingine mzuri," alisema Kamwe na kuongeza kwa siku tatu watakuwa na kazi ya kupokea wachezaji zoezi ambalo litaisha leo Jumatano.

"Tuna siku tatu hizi za kuripoti, kupima afya na mazoezi ya utimamu wa mwili, baada ya hapo tutakuwa na nafasi nzuri ya kutangaza 'programu' nzima ya Yanga kwenye maandalizi ya msimu ujao," alisema.

Akizungumzia ziara yao waliyoalikwa kwenda Afrika Kusini kwa ajili ya mechi ya Kombe la Toyota dhidi ya Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini katika mchezo utakaochezwa Julai 28, Uwanja wa Bloemfontein,  alisema itakuwa ni fursa nzuri kwao kutwaa taji la kwanza msimu ujao kabla ya hata michuano mingine haijaanza.

"Niwaambie tu watu kuwa mechi itakuwa ni moja tu, tukishinda tutachukua kombe letu, kabla ya mechi hiyo tutakuwa na wiki tatu za kunoa visu vyetu vizuri, na nadhani hilo litakuwa kombe letu la kwanza, tena tutalichukua nje ya nchi," alisema Kamwe.

Wakati hayo yakiendelea, klabu hiyo jana mchana imemtangaza mchezaji Aziz Andambwile akitoka Singida Fountain Gate.

Kiungo huyo mkabaji ambaye ni mzawa, alikuwa akiichezea Mbeya City, kabla ya kujiunga na Singida Big Stars mwaka  2022.

Usajili wa mchezaji unakuja siku moja, baada ya Simba kumsajili kiungo mkabaji kutoka klabu hiyo hiyo, Yusuph Kagoma.

Habari zinasema awali Yanga ilimhitaji Kagoma, lakini ilizidiwa kete na Wekundu wa Msimbazi na baadaye kuamua kumgeukia Andambwile.

"Tunashukuru, tumefanya usajili mzuri, tumesajili wachezaji bora na kutengeneza kikosi bora cha ushindani ndani na nje ya nchi, hatukuwa na kelele kwa sababu wachezaji tuliotaka kuwasajili safari hii ni wakubwa ambao tungeenda kwa kelele tungewapoteza, watu walikuja kushtuka mwishoni tumeshamaliza mchezo," alitamba Kamwe.