Yanga: Tutaishangaza Afrika

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 08:54 AM Mar 28 2024
Mashabiki wa Yanga wakishangilia timu yao katika moja ya michezo yao.
Picha: Yanga SC
Mashabiki wa Yanga wakishangilia timu yao katika moja ya michezo yao.

LICHA ya watangazaji na wachambuzi wa soka mbalimbali kutoipa Yanga nafasi ya kufanya vizuri katika mechi ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Mamelodi Sundowns kutoka Afrika Kusini, uongozi wa vinara hao wa Ligi Kuu Tanzania Bara umesema wataishangaza Afrika.

Yanga itawakaribisha Mamelodi Sundowns katika mechi ya kwanza ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika itakayochezwa keshokutwa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini, Dar es Salaam.

Ofisa Habari wa Yanga, Ali Kamwe, alisema jana mazoezi ya timu yake yanayoongozwa na Kocha Mkuu, Miguel Gamondi, yanawapa matumaini ya kuondoka na matokeo chanya katika mechi hiyo muhimu.

Kamwe alisema kikosi chao kipo tayari kuwavaa Mamelodi Sundowns na wanaamini watapata ushindi katika mchezo huo.

Alisema benchi la ufundi limekamilisha kila kitu kinachohitajika kuanzia kiufundi na kimbinu ili kupata ushindi, na kwa sasa wanasubiri kuona wachezaji wanafanya kile walichowaelekezwa kwenye uwanja wa mazoezi.

"Tangu Yanga imepangwa na Mamelodi Sundowns kwenye droo, nimeona watangazaji na wachambuzi hapa nchini na Afrika kwa ujumla kama vile hakuna kitu chochote kizuri ambacho timu yetu imefanya. Wao wanachokijua ni mambo mazuri ya wapinzani wetu, wanachofanya ni kuwataja wachezaji wazuri tu wa Wasauzi hao, kama vile sisi hatuna wachezaji bora.

Sasa tunawaambia tutakachowafanya Mamelodi hawataamini, ujumbe wa Jumamosi utakwenda kwa wote ambao hawaamini kama sisi tunaweza kuifunga timu hiyo, tunakwenda kuwaonyesha kuwa sisi ni wakubwa na tutaishangaza Afrika," alisema Kamwe.

Hata hivyo, wakati Yanga ikiendelea na hamasa, Kamwe amesema ameambiwa na Rais wa Yanga, Hersi Said, mwisho wa hamasa ni Alhamisi (leo), kwa ajili ya kupisha mechi nyingine ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika, kati ya wawakilishi wengine wa Tanzania, Simba dhidi ya Al Ahly ya Misri.

"Rais wa Yanga ameniambia tufanye hamasa kuanzia Jumanne, Jumatano na Alhamisi iwe mwisho, tuache Ijumaa na wenzetu nao wajulikane kama wamo na wana mechi kwa sababu hawajadiliwi, Afrika nzima inazungumza mechi hii (Yanga na Mamelodi Sundowns) na siyo yao," alisema Kamwe kwa namna ya utani wa jadi.

Kamwe alisema licha ya kutangaza kuingia bure katika eneo la mzunguko, lakini ulinzi utakuwa mkali, hivyo wamewataka mashabiki wasiogope kumiminika uwanjani.

"Msiwe na wasiwasi, mje ulinzi utakuwa mkali, ila tunachotaka kuwaambia wanachama na mashabiki wa Yanga, mechi hii itakuwa na mashabiki wengi kutoka mataifa mengi mbalimbali, hivyo kila mmoja akiwa uwanjani, ahakikishe anajali usalama wa mwenzake," alisema ofisa huyo.

Hii ni mara ya kwanza kwa Yanga kucheza hatua ya robo fainali Ligi ya Mabingwa tangu kuanza kwa muundo huo mwaka 1997, huku ikiwa imejidhatiti kusonga mbele.

Baada ya mechi ya keshokutwa, timu hizo zitakutana Afrika Kusini katika mchezo wa marudiano utakaochezwa Aprili 5, mwaka huu kwenye Uwanja wa Loftus Versfield ulioko Pretoria.

Yanga bado inashiriki mashindano hayo yanayoandaliwa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF), ikiwa na kumbukumbu ya kucheza fainali ya michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika msimu uliopita, ilipoteza dhidi ya wenyeji USM Alger ya Algeria.