TCRA: Siku ya Wasichana na TEHAMA, utumika kuwahamasisha kusoma masomo ya sayansi

By Cynthia Mwilolezi , Nipashe
Published at 05:33 PM Apr 25 2024
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TRCA), Dk.Jabir Bakari.
Picha: Mpigapicha Wetu
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TRCA), Dk.Jabir Bakari.

MKURUGENZI Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TRCA),Dk.Jabir Bakari,amesema kila mwaka wanatumia maadhimisho ya siku ya Kimataifa ya Wasichana na TEHAMA, kuhamasisha wasichana kuchukua masomo ya sayansi,uhandisi,teknolojia na hisabati ili kuwaandaa kuja kunufaika na fursa zilizopo.

Akizungumza leo jijini Arusha,katika maadhimisho hayo yenye  kauli mbiu isemayo "Uongozi", Dk.Jabir amesema  maendeleo ya dunia ya sasa, yameshikiliwa sana na matumizi ya teknolojia katika kila nyanja.

"Kwa hiyo  ni muhimu wasichana kujikita katika utengenezaji wa mifumo na programu za kiteknolojia,kusoma masomo ya uhandisi,kujikita katika tafiti mpya kama vile akili bandia na kuwa sehemu ya utaalam wa masomo ya Tehama, kwa ngazi za elimu na pia kuja kushiriki katika ngazi ya kutunga sera,hasa katika eneo hili la Tehama,"amesema.

Amrsema sekta ya mawasiliano ya simu nchini, imeendelea kukua kwa kasi ambapo hadi Machi mwaka huu, laini za simu zilikuwepo milioni 72.5  toka laini milioni 64.1 mwezi Juni, 2023 sawa na ongezeko la asilimia 13.

Alisema takwimu hizo za Machi zimeonyesha ongezeko la watumiaji wa intaneti kwa asilimia 8.2 toka watumiaji  milioni 34 Juni mwaka jana, hadi kufikia watumiaji milioni 36.8.

"Sababu zilizochangia ongezeko hilo ni matumizi ya intaneti,ambayo yamechangia kuwa na maudhui mengi ya Kiswahili,uwekezaji mkubwa kwenye miundombinu iliyofanyika kwenye maeneo mbalimbali,simu janja zimeongezeka kutoka milioni 16.7  Juni mwaka 2023, hadi milioni 20.1,Machi mwaka huu ikiwa ni ongezeko la asilimia 20,"amesema.

Amesema akaunti za fedha za simu za mkononi zimeongezeka kutoka akaunti milioni 47.3 mwaka jana hadi kufikia milioni 53 mwaka huu na ongezeko kubwa la miamala ya fedha kutoka milioni 420 mwaka jana hadi kufikia milioni 473 mwaka huu.

Naye Naibu Waziri wa Habari,Mawasiliano na Teknolojia ya Habari ,Mhandisi Maryprisca Mahundi amesema Tanzania imepiga hatua kubwa kwenye utoaji wa huduma za mawasiliano kwa gharama nafuu kwa watu wa kijini na vijijini kwa kufanikisha kutoa laini za simu milioni 72.5 hadi kufikia Machi mwaka huu, ukilinganisha na nchi zingine.

Pia amesema katika kipindi hicho idadi ya watumiaji wa mitandao ya Internet imekuwa hadi kufikia watu milioni 36.8 na kufanikisha waranzania wengi kuashiriki ipasavyo uchumi wa kidijiti.