Korti yaamuru Selasini kumlipa Mbatia mil. 80/-

By Grace Gurisha , Nipashe
Published at 07:27 AM May 04 2024
news
Picha: Maktaba
Aliyekuwa Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia.

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam imemtaka Makamu Mwenyekiti wa Chama cha NCCR-Mageuzi, Joseph Selasini, kumlipa fidia ya Sh. milioni 80 aliyekuwa mwenyekiti wa chama hicho, James Mbatia.

 Selasini ametakiwa kumlipa fidia hiyo Mbatia kutokana na kumchafua kuwa aliwaomba rushwa Suzan Masele na Joyce Sokombi ili wateuliwe wabunge wa viti maalum.

 Mahakama hiyo ilifikia uamuzi huo baada ya kujiridhisha kwamba maneno aliyoyatoa Selasini yalikuwa ya udhalilishaji na pia imemtaka ama aende Musoma alikotoa maneno hayo au kuomba radhi kwenye gazeti linalosambazwa eneo kubwa la nchi katika ukurasa wa mbele.

 Uamuzi huo ulitolewa juzi na Hakimu Mkazi Mkuu, Aaron Lyamuya, katika Shauri la Madai Na. 87/2023 lililofunguliwa na Mbatia dhidi ya Selasini, akimtaka amlipe fidia ya Sh. milioni 500 kwa kumchafua.

 Hakimu Lyamuya alisema mahakama imejiridhisha kwamba maneno aliyoyatamka Selesani yalikuwa ya udhalilishaji kwa kuwa yalikuwa yana viashiria vya jinai kwa sababu yalikuwa yanahusisha tuhuma za rushwa.

 Kutokana na kujiridhisha huko, alimwamuru Selasini aombe radhi kwa njia mbili, ama  arudi Musoma alikofanyia kikao cha kumchafua ili aombe radhi au aombe radhi kwenye gazeti lolote linalosambazwa eneo kubwa la nchi ukurasa wa mbele na kumlipa amlipe Sh milioni 80 fidia kwa kumdhalilisha.

 Pia mahakama hiyo imetoa zuio kwa Selasini au mtu yeyote kutoa maneno ya udhalilishaji dhidi yake na pia Selasini anatakiwa kulipa gharama za shauri hilo.

 Ilidaiwa kuwa maneno hayo ya udhalilishaji, Selasini aliyoyatoa katika kikao kilichofanyika nyumbani kwa Mzee Chimera eneo la Mlango Mmoja, Kata ya Nyasho mkoani Mara.

 Alidai kwamba Mbatia alipokea fedha kutoka kwa Susan Masele Sh. milioni 70 na Joyce Sokombi Sh. milioni 30 ili kuteuliwa wabunge wa viti maalum.

 Katika maombi yake, Mbatia  aliiomba mahakama kwamba Selasini amwombe radhi kwa kumchafua, alipwe fidia ya Sh. milioni 500 na itoe amri ya zuio kwa mtu yeyote au kwa Selesini kuendelea kumchafua. Pia aliomba gharama za kesi alipe mlalamikiwa (Selasini).

 Akizungumza nje ya mahakama jana, Wakili wa Mbatia, Hudson Mchau, alisema  wamefika mahakamani hapo kwa ajili ya kuleta barua kuomba nakala ya hukumu kwa ajili ya kufungua maombi ya utekelezaji ya uamuzi huo pamoja na gharama za shauri hilo.