ACT yahofia kupanda bei za vyakula

By Beatrice Shayo , Nipashe
Published at 08:36 AM May 04 2024
Waziri Kivuli wa Kilimo, Umwagiliaji na Maendeleo ya Ushirika wa Chama cha ACT-Wazalendo, Mtutura Abdallah.
Picha: Mpigapicha Wetu
Waziri Kivuli wa Kilimo, Umwagiliaji na Maendeleo ya Ushirika wa Chama cha ACT-Wazalendo, Mtutura Abdallah.

WAZIRI Kivuli wa Kilimo, Umwagiliaji na Maendeleo ya Ushirika wa Chama cha ACT-Wazalendo, Mtutura Abdallah, amesema endapo bajeti ya kilimo haitaongezwa kwa mwaka wa fedha 2024/25, bei za vyakula zinaendelea kupanda na kuathiri maisha ya watanzania.

Abdallah aliyasema hayo jana jijini Dar es Salaam wakati  chama hicho kikichambua bajeti ya kilimo iliyowasilishwa bungeni juzi.

Alisema bajeti ya kilimo isipoongezwa hususani kuiwezesha Wakala wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) kununua na kuhifadhi chakula cha kutosha,  bei ya vyakula itapanda.

“Bado miradi mingi ya umwagiliaji ipo katika hatua ya ndoto na hata iliyokwisha kuanza, kutekelezwa wake ni sawa na mwendo wa konokono,” alisema.

Abdallah alisema Tanzania inaendelea kutegemea sekta ya kilimo katika ukuaji wa uchumi na maendeleo ya wananchi wake kwa kutoa ajira kwa asilimia 61.1 ya nguvu kazi, na inachangia zaidi ya asilimia 100 ya chakula kinachopatikana nchini.

Alisema mpango wa bajeti unapaswa kubeba dhima hiyo ya kukabiliana na changamoto za uzalishaji, uhifadhi na mauzo ya chakula.

“Wanatakiwa kuhakikisha wakulima wanapata kwa wakati pembejeo za kilimo kwa kuwekeza ruzuku, ili kuwawezesha kumudu gharama na kuongeza tija katika uzalishaji,”alisema.

Alisema mikakati ya kilimo lazima ifungamanishwe na viwanda ili kuongeza thamani, kuongeza uzalishaji na kuhakikisha kunakuwa na masoko ya uhakika ya bidhaa za mauzo ndani ya nchini na ziada kusafirishwa nje.

Abdallah aliihatarisha serikali kuruhusu mbegu za GMO kuwa ni kusababisha kifo cha mbegu na chakula asili ambazo ndiyo tegemezi kwa wakulima wadogo vijijini ambao hawataweza kumudu gharama za kununua mbegu za GMO kila msimu wa kilimo.

Aidha, aliitaka serikali itoe tamko la kusitisha msimamo wake wa kutokuendelea na utafiti unahusiana na mbegu za GMO, na ihakikishe wakulima wa Tanzania wanalindwa dhidi ya mbegu hatari zitakapoanza kutumika  kwa kuwa, katika nchi za jirani wamesikia zikiruhusiwa.

“Matumizi ya mbegu za GMO zimekuwa zikipingwa katika nchi nyingine hata za Ulaya, ambapo matumizi yake yalianza. Serikali ihakikishe sekta ya kilimo inafanya mageuzi yatakayowalinda wakulima wadogo,” alisema.

Alisema mfumo wa stakabadhi ghalani umekuwa ni kitanzi kwa wakulima na kuwaachia maumivu makubwa, badala ya kuwa msaada kama ambavyo ilitarajiwa.

Abdalah alisema changamoto ya mfumo huo, hakuna ushirikishwaji wa moja kwa moja kuhusu kuamua bei ya mazao ya wakulima, na ucheleweshaji wa malipo kwa wakulima, jambo ambalo wakulima wengi hawawezi kumudu na kujikuta wakiuza kwa watu wa kati.

“Tumeangalia bajeti na vipaumbele vyake vya wizara, hatujaona mkakati wa kuboresha mfumo huo, ili kuwezesha na kuwanufaisha wakulima, tunataka huu mfumo uimarishwe uwe wa kieletroniki na uwe wa papo kwa papo,”.

Abdalah aliitaka serikali kueleza fedha za ruzuku zimepelekwa wapi, ikiwa wakulima hawajanufaika nayo.

Alisema ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), inaonyesha wakulima milioni 2.55 kati ya milioni 3.4, waliosajiliwa katika mpango wa ruzuku sawa na asilimia 75, hawakupata wala kutumia mbolea kupitia mpango wa ruzuku, licha ya kuwa na sifa ya kupatiwa mbolea hiyo ya ruzuku.

Alisema ACT inaitaka serikali kuingilia kati mfumo wa uagizaji na usambazaji kwa kuiwezesha kibajeti kampuni ya taifa ya Mbolea (TFC), kuagiza nje na kusambaza mbolea nchini, ili kuongeza uwezo wa usambazaji wa mbolea unaotokana na kulegalega.

Abdallah alisema wanachokitaka ni serikali irejeshe mfumo wa uagizaji wa mbolea, kulipa madeni ya wasambazaji wa mbolea na kuondoa utegemezi wa mbolea kutoka nje ya nchi kwa kuweka mazingira rafiki ya uwekezaji ili watu kujenga viwanda.