Wabunge wataka bei elekezi ununuzi mazao kwa wakulima

By Vitus Audax , Nipashe
Published at 08:50 AM May 04 2024
Mbunge wa Viti Maalum (CCM), Jacqueline Msongozi.
Picha: Tovuti ya Bunge
Mbunge wa Viti Maalum (CCM), Jacqueline Msongozi.

SERIKALI imeombwa kuja na mpango mkakati wa kuweka na kusimamia utekelezaji wa bei elekezi za kununua mazao kutoka kwa wakulima ili kuokoa uchumi wao hususani kahawa na mahindi yanayouzwa kwa hasara na kutofautiana baadhi ya maeneo.

Wakichangia hoja katika makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Kilimo ya mwaka 2024/25, baadhi ya wabunge walisema, licha ya mazao yao kuwa na thamani kubwa yamekuwa yakinunuliwa kwa bei ya hasara kutoka kwa wakulima.

Kuhusu mahindi, Mbunge wa Viti Maalum (CCM), Jacqueline Msongozi, alisema zao hilo  limekuwa tofauti katika maeneo mbalimbali hususan katika kipindi cha mavuno na kusababisha hasara wakulima kutokana na kununua pembejeo kwa bei elekezi ambayo ni moja katika maeneo yote.

Alitoa mfano katika maeneo ya Songwe ambako alisema zao hilo linanunuliwa kutoka kwa wakulima kupitia bei iliyowekwa na Wakala wa Taifa wa Kuhifadhi Chakula (NFRA) ya Sh.1,000 kwa kilo moja, huku Ruvuma ikiwa ni Sh. 750.

“Wote wanawekewa ruzuku katika mbolea, pembejeo zinaletwa kwa bei sawa, sasa kwa nini maeneo mengine yanunuliwe kwa bei juu na kwingine chini, weka uwiano wa ununuzi inaweza kuwa tofauti, lakini isiwe kubwa kama ilivyo sasa,” alisema.

Mbunge wa Moshi Vijijini (CCM), Prof. Patrick Ndakidemi, alisema bei ambayo hahawa inanunuliwa kutoka kwa mkulima ni ndogo kuliko soko la kahawa lilivyo duniani.

Alisema kahawa ni zao maarufu duniani likishika nafasi ya pili na ina wakulima zaidi ya milioni 25 Tanzania ikiwa miongoni ambao ni wadogowadogo wanaozalisha asilimia 80 ya zao hilo duniani, licha ya kuwa na maisha magumu.

“Bei wanazopata ni ndogo kulinganisha na thamani ya zao lenyewe, na hazitoshelezi kulingana na kazi kubwa ya uandaaji wa zao hilo. Maana kwa kahawa aina ya Robusta kilo moja ni Sh. 2,000, huku Arabica ikiwa ni Sh.3000,” alisema.

Mbunge Ndekidemi alisema kilo hiyo inayouzwa kwa bei hiyo ikienda nje inazalisha vikombe 120 hadi 140 vya kahawa, huku bei ya kikombe kimoja cha kahawa, ikiwa ni Dola za Marekani 3.5 hadi 3.7 sawa na Sh. 8,750 hadi 9,300  kwa kilo moja (sawa na zaidi ya Sh. milioni 1.05 hadi 1.3).

“Kwa hiyo hapa inaonekana kuwa, bei ya mkulima anayouza kilo moja ya kahawa ni sawa sehemu kidogo ya kikombe kimoja cha kahawa anayoiuza,” alifafanua.

Mbunge huyo aliishauri serikali kusaidia wananchi kupata masoko ya uhakika wa zao hilo na siyo kuendelea kuuza kwa bei ya hasara, ili kukabiliana na ukiritimba unaoendelea.

Aliitaka serikali iwashawishi wawekezaji wa uhakika kuja kuwekeza nchini viwanda vya uchakataji wa zao hilo ili kuuza bidhaa zilizochakatwa.

Mbunge wa Muleba Kasikazini (CCM), Charles Mwijage, aliishauri serikali kubaini na kutunza maeneo ya uzalishaji wa mazao muhimu nchini ikiwamo kahawa na zababu ili yasiathiriwe na maendeleo pamoja na ukuaji wa kidemgraphia.

Mbunge wa Viti Maalum (CHADEMA), Sophia Mwakagenda, alisema wakulima wa parachichi wilayani Lungwe pamoja na maeneo mengine wanadhurumiwa haki zao kupitia mizani inayotumiwa na madalali wakati wa manunuzi ya zao hilo.

 Aliitaka serikali kuingilia kati suala hilo na kuanza kwenda kwa wakulima na kupima na kununua yenyewe mazao hayo na kuacha kuwatumia madalali hao ambao wanawaumiza.

“Mizani inayotumika ununuzi mazao kutoka kwa wakulima itazamwe na kurekebishwa, kwani wakulima wanatoka kwenye maeneo yao wakiwa wamepima vyema mazao yao, wakifika kwa wanunuzi vipimo vinapungua kwa kilo kuanzia tano, hali ambayo inazidi kuwaumiza,” Mbunge Viti Maalum (CCM), Bupe Mwakang’ata alisema.