Dk. Yonazi atoa pole kwa waathirika wa maafa Moshi

By Maulid Mmbaga , Nipashe
Published at 03:09 PM May 04 2024
Sehemu nyumba iliyoathirika na mafuriko.
Picha: Maktaba
Sehemu nyumba iliyoathirika na mafuriko.

KATIBU Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Bunge na Uratibu Dk. Jim Yonazi ametoa salamu za pole kwa familia iliyopatwa na msiba wa ndugu wanne waliofariki kwa kuangukiwa na nyumba kutokana na maporomoko ya udongo na mawe yaliyosababishwa na mvua zinazoendelea kunyesha.

Dk. Yonazi amefika leo katika makazi ya familia hiyo iliyoko Kata ya Kimochi Kijiji cha Lyakombila Wilaya ya Moshi Vijijini Mkoani, ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya kikazi ya kujionea hali halisi ya madhara yatokanayo na mvua zinazoendela kunyesha katika maeneo mbalimbali ya nchini.

Baada ya kukagua makazi yaliyoathiriwa na mvua hizo, miundombinu ya barabara pamoja na madaraja, Dk. Yonazi ametoa rai kwa kila mwananchi kuwa mstari wa mbele katika masuala ya maafa kwa kuzingatia madhara  yatokanayo na mafuriko ikiwemo uharibifu wa miundombinu, mazao pamoja na vifo.

“Serikali inatoa pole kwa familia hii iliyofikwa na msiba mzito wa kuondokewa na baba, mtoto, kaka pamoja na mjukuu baada ya  kuanguikiwa na maporomoko kutoka katika milima na kupelekea umauti, hili ni pigo na tunatoa pole, Mungu aendelee kufariji familia na sisi tupo pamoja nanyi katika wakati huu wa majonzi,” amesema Dk. Yonazi

Pia katibu huyo amezitembelea Kambi maalum ikiwemo ya Lucy Lameck na kambi ya shule ya msingi Ghona zilizotengwa kwa lengo la kutoa huduma muhimu kwa waathirika wa maafa hayo ikiwemo wa kata ya Saranga na Mji Mpya huku akiwasihi kuendelea kuwa watulivu na kuiunga mkono serikali katika hatua zote za masuala ya mejenimenti ya maafa.

Mkuu wa Wilaya ya Moshi Zephania Sumaye, amesema serikali imeendelea na hatua mbalimbali za kusaidia waliopatwa na madhara ya maafa ya mafuriko ikiwemo kuwahudumia katika kambi zilizotengwa, kutoa elimu ya taadhari za mvua zinazoendelea kunyesha na kuwahimiza wananchi kuendelea kuchukua tahadhari na kuhama maeneo hatarishi.

"Lengo ni kuwa na jamii salama na stahimilivu dhidi ya maafa na kuendelea na shughuli za uzalishaji ili kujiletea maendeleo yao na Taifa kwa ujumla," amesema Sumaye.