Ustawi wa Jamii waadhimisha Miaka 60 ya Muungano,Butiku awapa somo

By Sabato Kasika , Nipashe
Published at 03:41 PM Apr 25 2024
Mwenyekiti wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere Foundation, Joseph Butiku.
Picha: Sabato Kasika
Mwenyekiti wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere Foundation, Joseph Butiku.

CHUO Cha Ustawi wa Jamii kimefanya kongamano la miaka 60 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ili kujengea wanafunzi wake uelewa kuhusu umuhimu wa muungano huo.

Kongamano hilo limefanyika leo chuoni hapo na kushirikisha watu mbalimbali akiwamo Mwenyekiti wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere Foundation, Joseph Butiku.

Akimkaribisha Butiku ambaye alikuwa mgeni rasmi katika kongamano hilo, mkuu huyo wa chuo amesema tangu kuanzishwa muungano miaka 60 iliyopita, kuna kundi kubwa la Watanzania linahitaji kuujua.

"Tumekualika mzee Butiku kwa sababu unakuja vizuri, hivyo ninaamini watu wengi watafaidika na kuwapo kwako katika kongamano hilo," amesema.

Akizungumza katika kongamano hilo, Butiku amesema,  muungano huo sio wa Nyerere na Karume bali ni wa wananchi wa pande mbili.

"Nyerere na Karume walionyesha njia kisha wananchi wakaikubali, ndipo nchi zikaungana, wananchi walikuwa na uwezo wa kuukataa, lakini wakaikubali, hivyo ni wa kwao," amesema Butiku.
Dk. Peter Mgawe kutoka chuo hicho, amesema amani, mshikamano vimekuwa nguzo ya maendeleo ya taifa ndani ya muungano huo.

"Vilevile, Kiswahili kimesaidia kuimarisha muungano ambao sasa imetimiza miaka 60 tangu uanzishwe," amesema Dk. Mgawe.

Mhadhiri wa Chuo cha Diplomasia, Abbas Mwalimu, alisema jiografia ndio ilisababisha wazungu  wawagawanye Watanganyika na Wazanzibar.

"Viongsozi wetu, Mwalimu Nyerere na Karume wakaamua  kuunganisha jamii yetu ambayo iligawanywa kwa sababu za kijiografia na sasa muungano wetu unaendelea," amesema Mwalimu.