Yanga: Copco FC mtatusamehe

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 12:09 PM Jan 25 2025
Kocha Mkuu wa Yanga, Sead Ramovic.
Picha:Mtandao
Kocha Mkuu wa Yanga, Sead Ramovic.

NGUVU, utulivu na kuweka dharau pembeni ndio kipaumbele cha mabingwa watetezi, Yanga kuelekea mechi ya raundi ya tatu ya mashindano ya Kombe la FA dhidi ya Copco FC itakayochezwa leo kwenye Uwanja wa KMC Complex, Dar es Salaam.

Yanga itashuka katika mchezo huo ikiwa na kumbukumbu ya kuondolewa kwenye michuano ya kimataifa ya Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya kushindwa kupata ushindi walipowakaribisha MC Alger kutoka Algeria.

Akizungumza kuhusu mechi hiyo, Kocha Mkuu wa Yanga, Sead Ramovic, alisema amejipanga kuingia uwanjani  kucheza kwa nguvu na kasi kama walivyokuwa wakicheza katika michezo ya mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika na Ligi Kuu Tanzania Bara.

Ramovic alisema asitokee mtu au wapinzani wao wakadhani ataidharau mechi hiyo, badala yake ameelekeza nguvu 'kubwa' kwa kutumia silaha zote ili kushinda mchezo huo.

"Tunatakiwa kushinda mechi hii, pia kushinda kombe hili, Yanga siku zote ni timu ya ushindi, tunakutana na timu hii ndogo, hatutaidharau, hatuwezi kudharau timu yoyote ile, tutacheza kama tutavyocheza mechi za Ligi ya Mabingwa Afrika na Ligi Kuu, kama tunavyocheza na timu yoyote kubwa, kwa nguvu kubwa, kwa kasi ya kutisha na kwa kutumia silaha zote tulizonazo ili kutinga hatua inayofuata," alisema Ramovic.

Naye Kocha Mkuu wa Copco yenye maskani yake jijini Mwanza, Lucas Mlingwa, alisema ataingia uwanjani akiwa na lengo la kutaka kutonesha kidonda ambacho kiliachwa na 'Waarabu.'

Mlingwa alikiri Yanga ni timu kubwa na bora, lakini wataingia na mkakati maalum, ambao utafanya kazi  waliokusudia ili kupata matokeo chanya.

"Tumejiandaa vya kutosha kwa ajili ya hii mechi, wachezaji wameniambia wako tayari kwa ajili ya kupambana na tunakwenda kucheza tukiwa na malengo ambayo tumejiwekea ili kuyatimiza kesho (leo).

Tunaamini Yanga ni timu bora, hilo kila mtu analijua na hiyo ni faida kubwa kwetu kucheza na mpinzani unayejua uwezo wa kiwango chake, huwezi kuingia kwenye Uwanja wa KMC Complex, kucheza nao mshindane, uwezo wa mchezaji mmoja mmoja, wana kiwango bora kuliko sisi, kwa maana hiyo tumekuja na mpango mkakati, yaani kufidia kile ambacho hatuna, kupunguza eneo lao la kucheza, sisi tuwe na namba kubwa ya watu katika kila eneo, ina maana wachezaji wetu ni lazima wakimbie sana," alisema kocha huyo.
Aliongeza wanahitaji kuendelea kupata matokeo mazuri msimu huu ili kuwaongezea uzoefu wachezaji wake.

"Msimu uliopita hautukufika hatua hii, tunaamini hadi hapa tulipo tumejifunza mengi, tunahitaji kupambana ili kuongeza jambo kwenye kikosi chetu, haitakuwa mechi rahisi kwa kila upande," aliongeza kocha huyo.

Katika mchezo wa leo, Yanga itatumia fursa kutaka kuwapoza na kuwafariji wanachama na mashabiki wao ambao wameumizwa na timu hiyo kushindwa kusonga mbele kwenye mashindano ya kimataifa yanayoandaliwa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF).

Ni mechi ya kiporo ambayo awali ilipaswa kufanyika Novemba, mwaka jana, lakini haikuchezwa kutokana na mabingwa hao watetezi kukabiliwa na michezo ya kimataifa.

Bingwa wa michuano hiyo hupata tiketi ya kuiwalilisha Tanzania Bara kwenye michuano ya kimataifa ya Kombe la Shirikisho Afrika.