Simba yatangaza rasmi kuachana na Kanoute

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 07:10 AM Jul 10 2024
Sadio Kanoute.
Picha: Mtandao
Sadio Kanoute.

KLABU ya Simba jana imetangaza rasmi kuachana na kiungo wake, Sadio Kanoute baada ya mkataba wake kumalizika klabu hapo.

Kanoute alijiunga na Simba msimu wa 2021/2022 akitokea kwenye klabu ya Al Ahly Benghazi ya nchini Libya na kusaini mkataba wa miaka mitatu uliomalizika hivi karibuni.

Hata hivyo, siku moja kabla ya kutangaza kuachana na Kanoute, uongozi wa klabu hiyo ulitangaza kumsajili kiungo mzawa, Yusuph Kagoma ambaye sasa anakwenda kuchukua nafasi ya Kanoute kwenye kikosi hicho.

Ofisa habari wa klabu hiyo, Ahmed Ally, alisema uongozi wa klabu hiyo unaendelea kukiimarisha kikosi chao kwa ajili ya msimu ujao wa Ligi na mshindano ya kimataifa watakayoshiriki.

"Tunamshukuru sana Kanoute kwa muda wote aliokuwa akiitumikia klabu yetu, mchango wake ni mkubwa mno na Wanasimba wataukumbuka," alisema Ahmed.

Aidha, alisema bado wanaendelea na usajili na hivi karibuni watatangaza mchezaji mwingine waliomsajili kwa ajili ya kuitumikia klabu hiyo.

"Simba ya msimu ujao itakuwa ya moto, tunataka kurudisha heshima yetu, tunataka kurudisha ufalme wetu na ndio maana unaona unafanyika usajili wa nguvu," alisema Ahmed.