Kundi la pili Simba kuondoka leo

By Faustine Feliciane ,, Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 07:42 AM Jul 10 2024
Ofisa habari wa klabu hiyo, Ahmed Ally
Picha: Mtandao
Ofisa habari wa klabu hiyo, Ahmed Ally

KUNDI la pili la wachezaji na viongozi wa klabu ya Simba linaondoka nchini leo kwenda Misri kuungana na wengine waliotangulia tayari kwa maandalizi ya msimu mpya.

Awali baadhi ya wachezaji na benchi la ufundi waliondoka nchini juzi kuelekea katika mji wa Ismailia watakapoweka kambi ya wiki tatu kabla ya kurejea nchini kwenye kilele cha tamasha la kila mwaka la 'Simba Day'.

Akizunguma na Nipashe, Ofisa habari wa klabu hiyo, Ahmed Ally, alisema baada ya kundi hilo la pili kuondoka sasa wataanza rasmi maandalizi yao chini ya kocha mpya Fadlu Davids aliyetangazwa na Simba hivi karibuni kuchukua mikoba ya kocha Benchikha aliyeachana na Simba.

"Sasa kikosi chetu kitakuwa kimekamilika tayari kwa maandalizi ya chini ya benchi jipya la ufundi, lakini golikipa wetu Ayoub Lakred naye ataungana na timu Misri akitokea kwao Morocco," alisema Ahmed.

Aidha, alisema kazi sasa imebaki kwa benchi la ufundi kuandaa timu tayari kwa mikikimikiki ya Ligi Kuu pamoja na mashindano ya kimataifa ambapo Simba itashiriki Kombe la Shirikisho Afrika.

Katika hatua nyingine, klabu hiyo imeweka mikakati ya kuwapima kilevi wachezaji wake wote watakaokuwa wakiingia kambini.

Habari zilizopatikana katika kikao kilichofanyika wiki hii kwenye hoteli moja pembeni ya Bahari ya Hindi, Dar es Salaam kilichoongozwa na Mwekezaji, Rais wa Heshima na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Klabu hiyo, Mohamed Dewji, pamoja na mambo mengine, kilisisitiza nidhamu kwa wachezaji pamoja na uwajibikaji ili kuipa mafanikio timu hiyo uwanjani.

Mmoja wa waliokuwa kwenye kikao hicho amesema, wachezaji wa timu hiyo walitangaziwa kuwa meneja mpya wa timu atakabidhiwa kifaa maalum kinachoweza kupima kama mchezaji ataingia kambini akiwa amelewa na kama itakuwa hivyo basi atazuiliwa kuingia kambini."

"Huu ni mkakati mpya wa kutengeneza timu ambayo ina wachezaji wenye nidhamu, mchezaji atapimwa na kifaa hicho, akionekana ana kilevi mwilini hatoruhusiwa kuingia kambini na hapo atakuwa amefanya makosa mawili, moja ni kutokuwa kwenye kituo chake cha kazi, lakini pia kuhesabiwa kuwa ni mlevi, hivyo atakumbana na adhabu kali ambayo itaainishwa baadaye," alisema mtoa taarifa huyo huku pia wachezaji wenye tabia ya ugomvi nao watakumbana na adhabu kama hiyo.

Pia katika kikao hicho kilichokutanisha Mwenyekiti, Bodi ya Wakurugenzi, Bodi ya Ushauri, wachezaji na baadhi ya wafanyakazi wa klabu hiyo, wametakiwa kuvaa nguo rasmi wakati wakiwa kambini ambazo ni zile zenye nembo ya wadhamini na ile ya klabu.