KOCHA Mkuu wa Simba, Fadlu David, ameonesha furaha kwa timu yake kupata ushindi wa mabao 5-2 dhidi ya Kagera Sugar, akisema ni mkubwa zaidi kuupata yeye kwenye Ligi Kuu tangu aanze kuifudisha timu hiyo, lakini akichukizwa na aina ya mabao ambayo wameruhusu dakika za mwishoni.
Akizungumza baada ya kumalizika kwa mchezo huo uliopigwa, Uwanja wa Kaitaba, Kagera, Fadlu alisema ushindi huo ulikuwa muhimu kwa kuwa ilikuwa ni mara ya kwanza kushinda hapo kwa misimu mitatu na mkubwa zaidi kwake, na timu kwa ujumla msimu huu, pia kuweka rekodi ya kuwa timu ya kwanza kushinda idadi kubwa ya mabao, lakini umeharibiwa na kuruhusu mabao mawili ambayo hayakuwa na ulazima wowote wa kutinga wavuni.
"Ninasema ninafuraha kwa ushindi kwa wachezaji wangu kufunga mabao matano, lakini nimehuzunishwa kuruhusu mabao mawili, haikubaliki, haifurahishi, ikikuwa ni mechi ya kuondoka na 'clean sheets'," alisema kocha huyo.
Alisema tatizo analoliona ni kwa wachezaji ambao waliingia kipindi cha pili ambao kwa sababu timu ilikuwa imeshashinda mabao manne, badala ya kwenda kupambana, wao walicheza kama wapo mazoezini.
"Akili ya wachezaji walioingia waliona mechi imeisha kwa hiyo waliingia na kucheza kama kukamilisha dakika, waliiweka timu matatizoni muda wote," alisema kocha huyo.
Alisema kwa timu ambayo inasaka pointi tatu na inasaka ubingwa haiwezi kuwa inaruhusu mabao kirahisi na kizembe namna ile, huku akisema anatarajia kukaa nao na kuwaeleza jambo hilo lisijirudia tena.
Yalikuwa ni mabao mawili ya Steve Mukwala, Fabrice Ngoma, Shomari Kapombe, na Jean Ahoua, yaliyoiwezesha Simba kupata ushindi huo kwa mara ya kwanza baada ya misimu mitatu, huku ikikwea juu ya msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara kwa kufikisha jumla ya pointi 34 na kuishusha Azam yenye pointi 33 iliyorudi nafasi ya pili.
Simba imecheza mechi 13, ikishinda michezo 11, sare moja na kupoteza moja, ikifunga mabao 29 na kuruhusu matano mpaka sasa, ikisalia na mechi mbili imalize mzunguko wa kwanza.
Katika hatua nyingine, mfungaji wa bao la kwanza, Kapombe, amempongeza mchezaji mwenzake Mohamed Hussein 'Tshabalala' kwa kumpa pasi ya bao, akisema amelipa ambacho kile yeye alikifanya misimu kadhaa iliyopita alipowahi kufanya hivyo.
"Nashukuru kwa kunipa pasi, lakini analipa kwa sababu mimi nimeshawahi kumpa pasi akafunga misimu kama miwili nyuma, anakumbuka mwenyewe," alisema Kapombe.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED