GOLIKIPA wa zamani wa Simba, Yanga, Azam FC, Deogratius Munishi 'Dida' na kiungo mkabaji, Said Makapu, wamejiunga na Geita Gold inayoshiriki Ligi ya Championship, imefahamika.
Geita Gold imewasajili wachezaji hao ili kuimarisha kikosi chao na hatimaye kufikia malengo ya kurejea Ligi Kuu Tanzania Bara msimu ujao.
Taarifa rasmi iliyotolewa na klabu hiyo jana imesema usajili wa nyota hao ulikamilika muda mfupi kabla ya dirisha la usajili kufungwa hapo Januari 15, mwaka huu, ambapo vilibaki vitu vichache tu vya kumalizia mchakato huo kabla ya kuwatangaza.
Klabu hiyo pia ilimtangaza Mohamed Muya, kuwa Kocha Mkuu wa kikosi hicho, akichukua nafasi ya Amani Josiah, ambaye kwa sasa amejiunga na Tanzania Prisons inayoshiriki Ligi Kuu Bara.
Muya ametua Geita Gold akitokea Fountain Gate, ambayo ilitangaza kumtimua muda mfupi baada ya kupokea kichapo kutoka kwa mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Yanga.
"Tunawatambulisha kwenu Dida, kipa mzoefu nchini, pia tunamleta kwenu Makapu, kiungo bora na mkongwe ambaye ataongeza nguvu katika kikosi chetu," ilisema sehemu ya taarifa hiyo.
Mbali na kuzidakia timu hizo, Dida pia amezichezea Mtibwa Sugar, Lipuli, Namungo na akacheza soka la kulipwa nchini Afrika Kusini katika timu ya University of Pretoria.
Dida, ambaye amewahi kuitumikia Timu ya Soka ya Taifa (Taifa Stars), ametua Geita Gold kama mchezaji huru.
Makapu, ambaye amesajili kutoka Mashujaa FC, amewahi kuichezea Yanga, mwaka 2022, kabla ya kwenda Singida Big Stars.
Hadi kumalizika kwa mzunguko wa kwanza wa Ligi ya Championship, Geita Gold, iliyoshuka daraja msimu uliopita, iko katika nafasi ya tatu ikiwa na pointi 33 nyuma ya vinara Mbeya City yenye pointi 34 wakati vinara ni Mtibwa Sugar yenye pointi 38.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED