CECAFA yambeba Karia CAF

By Somoe Ng'itu , Nipashe
Published at 11:38 AM Jan 25 2025
 Wallace Karia.
Picha: Mtandao
Wallace Karia.

WAJUMBE wa Mkutano Mkuu wa Baraza la Vyama vya Soka kwa Nchi za Afrika Mashariki na Kati (CECAFA), wamempitisha Rais wa baraza hilo, Wallace Karia, kuwa mgombea pekee wa nafasi ya Ujumbe wa Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF), imethibitishwa.

Uchaguzi Mkuu wa CAF unatarajiwa kufanyika Machi, mwaka huu nchini Morocco.

Karia, ambaye ni Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), alikuwa anatarajia kuchuana na Rais wa Shirikisho la Soka Uganda (FUFA), Moses Magogo.

"Magogo hatagombea nafasi ya ujumbe wa kamati ya utendaji ya CAF na sasa Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania, Wallace Karia atakuwa mgombea pekee wa nafasi hiyo. Maana yake tayari Karia ameshapita katika nafasi hiyo," chanzo chetu kilisema.

Karia pia amethibitishwa kuwa mgombea pekee wa nafasi ya Urais katika uchaguzi ujao wa TFF, utakaofanyika baadaye mwaka huu.

Wajumbe wa Mkutano Mkuu wa TFF, waliazimia hivyo katika mkutano wa mwaka uliofanyika Desemba 21, mwaka jana mkoani Kilimanjaro.

CECAFA pia imetangaza kumuunga mkono Rais wa Shirikisho la Soka la Djibouti, Souleiman Waberi, kuwania nafasi ya ujumbe wa Kamati ya Utendaji wa FIFA, ambayo pia itafanya uchaguzi wake baadaye mwaka huu.

Waberi, mwamuzi wa zamani wa kimataifa, kwa sasa ni Makamu wa Tatu wa Rais wa CAF.