Azam yampiga bei Kipre Junior MC Alger, Fei Toto bado yupo

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 07:23 AM Jul 02 2024
Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano ya Azam, Thabit Zacharia.
Picha: Mpigapicha Wetu
Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano ya Azam, Thabit Zacharia.

KLABU ya Azam imethibitisha kuwa imefikia makubaliano na MC Alger ya Algeria kuwauzia mchezaji wao, Kipre Junior, raia wa Ivory Coast kwa kiasi cha Dola 300,000 za Kimarekani sawa na Sh. milioni 824 za Tanzania.

Klabu hiyo imesema hayo baada ya kuzuka tetesi hivi karibuni kuwa mchezaji huyo anayecheza nafasi ya winga zote mbili na kiungo mshambuliaji kutakiwa na klabu hiyo.

Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano ya Azam, Thabit Zacharia maarufu Zaka Zakazi, amesema jana kuwa mazungumzo ya pande zote mbili yamekamilika na kilichobaki sasa ni kuandikishiana mikataba.

"Ni kweli MC Alger wametuma ofa yakafanyika mazungumzo marefu baina yetu na wao na kufikia muafaka, ninavyokwambia ni kwamba muafaka umefikiwa, kilichobakia ni taratibu zingine kwamba huyu bwana anaondoka, klabu imeshakubali ila kilichobaki ni kuandikishiana mikataba ndiyo hatua zinazofuata," alisema Zaka Zakazi.

Hata hivyo, alisema haikuwa nia ya klabu kumuuza, ila klabu hiyo ya Algeria imekubali kutoa kiasi hicho kilichowekwa kwenye mkataba baina ya Azam na mchezaji huyo kama ikitokea timu inayomtaka.

"Tunamuuza pesa nyingi sana, sisi tukiwasajili wachezaji kwenye mikataba tunaweka kipengele cha pesa ambayo anaweza kuuzwa, huyu tuliweka dola 300,000 za Kimarekani na jamaa wameweka huo mzigo, hapo huwezi kusema chochote, labda mchezaji tu akatae," alisema.

Kipre alikuwa amebakisha mwaka mmoja na Klabu ya Azam, akisajiliwa misimu miwili iliyopita kutoka Sol FC ya Ivory Coast.

Msimu uliomalizika amehusika na mabao 18, akifunga tisa na kutoa pasi za mwisho tisa, na kuwa kinara wa 'asisti' kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara msimu wa 2023/24.

Aidha, Zaka alikiri Klabu ya Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini kutaka kumtwaa kiungo mshambuliaji wao tegemeo, Feisal Salum, lakini hawakufika kile kiwango walichokiweka cha kuvunja mkataba.

"Nayo ni kweli, ila niwakumbushe watu kuwa wachezaji wetu hawapo sokoni, hata Kipre hatukuwa tunamuuza ila ukiwataka fikia malipo yalivyoandikwa kwenye mkataba, yaani kile kipengele cha pesa tulichoweka, MC Alger wamefikia, ila Mamelodi Sundowns wao hawakufikia hicho kiwango kwa hiyo Fei Toto bado yupo," alisema Zaka.