Rais Mwinyi mgeni rasmi mbio za Tigo-Zantel 2024

By Faustine Feliciane , Nipashe
Published at 08:30 AM Oct 31 2024
Rais wa Zanzibar, Dk. Hussein Ali Mwinyi.
Picha: Mtandao
Rais wa Zanzibar, Dk. Hussein Ali Mwinyi.

RAIS wa Zanzibar, Dk. Hussein Ali Mwinyi, anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika Tigo-Zantel Zanzibar Marathon 2024 zilizopangwa kufanyika keshokutwa visiwani humo.

Huu ni msimu wa nne mfululizo wa mbio hizo zinazotarajiwa kushirikisha wanariadha kutoka sehemu mbalimbali ndani na nje ya Tanzania ambao watashindana kuanzia umbali wa kilomita tano, kilomita 10 na kilometa 21 (nusu marathon).

Mkurugenzi wa Tigo- Zantel upande wa Zanzibar, Azizi Said Ali, alisema jijini jana kuwa maandalizi ya mbio hizo yanaendelea vizuri na tayari washiriki  wameanza kujiandikisha kwenye vituo vilivyoko Dar es Salaam na Zanzibar.

Ali alisema Rais Mwinyi amethibitisha  atakuwa mgeni rasmi katika mbio za mwaka huu.

"Ni jambo la kujivunia kuona mkuu wa nchi anatambua faida ya watu kushiriki kwenye mazoezi na mashindano kama haya, siku ya mbio tunatarajia Rais Mwinyi kuwa mgeni rasmi," alisema Ali.

Alisema wanatarajia leo kuanza kupokea washiriki kutoka nje ya Zanzibar tayari kwa ajili ya kushiriki katika mbio hizo ambazo zitachochea uchumi wa wafanyabiashara na wajasiriamali.

"Muda wa kujiandikisha unaenda ukingoni, ambao bado wajitokeze, tunatarajia kuwa na idadi kubwa ya washiriki, wapo ambao wanatoka Kenya tayari wamethibitisha kushiriki na wamejiandikisha tayari," alisema mkurugenzi huyo.

Aliongeza ili kuzifanya mbio hizo kuwa katika kiwango cha juu, wamefanya maboresho mbalimbali kwa lengo la  kuhamasisha watu wajitokeze kwa wingi  kushiriki.

"Tunawaomba watu wajitokeze kujiandikisha na kushiriki mbio hizi, muda bado upo, unaposhiriki unajiweka katika mazingira mazuri ya kuimarisha afya yako," aliongeza.