Wafanyabiashara watengewe maeneo ya uhakika wa kudumu

Nipashe
Published at 10:23 AM Jul 10 2024
Wamachinga wa Simu 2000.
Picha: Mtandao
Wamachinga wa Simu 2000.

WAFANYABIASHARA wadogo au wamachinga wanaouza bidhaa mbalimbali mijini na kwenye majiji ni waathirika wa majanga mengi.

Mosi, moto unaoteketeza mali zao, kadhalika kuhamishwa mara kwa mara kwenye maeneo waliyohamishiwa.

Adha wanazokumbana nazo ni wakati mwingine kupata vipigo na kupoteza mali zao wakati wanapokaidi kuhama maeneo hayo. Katika matukio hayo kuna wengine waliopoteza maisha katika heka heka hizo.

Ni kutokana na mali zao kuteketea, kuibwa, kubomolewa maduka na vibanda na masuala yanayofanana na hayo katika masoko mbalimbali nchini.

Inaumiza kuona mtu aliyejitahidi kutafuta mtaji kwa shida na baadaye anapofungua biashara yake na kuanza kutengemaa anatakiwa kuondoka na wakati mwingine kwa kuvunjiwa vibanda vyao.

Wamachinga wa soko la Simu 2000 au kituo cha mabasi cha Mawasiliano kilichoko Ubungo Dar es Salaam, hoja yao ni kuwa walihamishiwa hapo na kuhakikishiwa hawatabugudhiwa.

Taarifa za kuwahamisha kutoka kituoni hapo kwa maelezo kuwa soko hilo limetolewa kwa kampuni ya mabasi yaendayo kasi ili kujenga karakana, zimewafanya kuzua sintofahamu hiyo.

Tumewasikia wafanyabiashara hao wakisema wanataka kusikilizwa na kuamuliwa hatima yao ili ieleweke.

Wamachinga wa Simu 2000, wanasikika wakisema wamekaa katika eneo hilo baada ya kuhamishwa kutoka maeneo mengine wakiambiwa kuwa kituo cha Mawasiliano kitakuwa cha kudumu.

Ni wazi kuwa wanaofaidika na masoko Dar es Salaam ni wafanyabiashara mbalimbali kutoka Tanzania nzima, wanaoleta bidhaa zao mijini kwenye mahitaji makubwa.

Ni uchumi wa nchi na pia ni maisha ya Watanzania.

Soko la Simu 2000 ni mali ya serikali na wafanyabiashara hao wanatakiwa kusikiliza na kuheshimu serikali ambayo ndiyo inayosimamia ardhi kwa maendeleo ya taifa.

Lakini ni lazima pia kuangalia hatima ya wamachinga hao ambao wamejiajiri ili kumudu maisha yao.
 Serikali imeahidi kukaa nao Jumamosi ni jambo jema, lakini kuja na ufumbuzi wa kudumu wa masoko ya wamachinga kwenye majiji na miji ndicho kitu muhimu zaidi.

Wamachinga wafahamu wanakwenda wapi kufanya biashara zao, kwa utaratibu wa kumudu maisha yao.

Wafanyabiashara hao wanalalamika kwamba hawakupewa notisi na kwamba wamesikia kuhusu uhamisho wao kwenye mitandao na kutaka haki itendeke.

Masuala yanayogusa maisha ya watu moja kwa moja kama ajira yaangaliwe kwa umakini mkubwa.

Tunajua soko la Mawasiliano au Simu 2000 ni sehemu watu walipojiajiri ndiko uliko mkate wao wa kila siku, ingekuwa vyema wakashirikishwa kwenye kufikia maamuzi badala ya kuyasikia mitandaoni.

Tunajua lengo la serikali ni jema la uamuzi wa kukabiliana na foleni na kurahisisha usafiri Dar es Salaam, maamuzi hayo yanahitaji kuyatafakari na kushirikisha pande zote tena ziridhike ili kuepusha taharuki.

Serikali ina maeneo mengi na pia ina uwezo wa kuweka kitega uchumi popote hivyo si vibaya ikatafakari kupeleka karakana hiyo eneo lisilo na wafanyabiashara ili kuepusha migogoro.

Baadhi ya sehemu ni Kimara Temboni ambako ipo sehemu iliyofungiwa inayohifadhi magari mabovu, ikisimamiwa na Wakala wa Taifa wa Barabara –TANROADS.

Tunawasihi wafanyabiashara hao kusikilizwa na kuwasiliana na serikali ili kuwa na mchakato wenye amani unaowanufaisha pia ukilinda maslahi ya taifa.