KILICHOONEKA katika mechi ya nusu fainali Ngao ya Jamii, ni kwamba ni waamuzi ndiyo waliokuwa na presha na mchezo wenyewe kuliko hata wachezaji.
Wachezaji walikuwa wakicheza kwa kufuata maelekezo ya walimu wao jambo ambalo lilionekana dhahiri machoni mwa mashabiki wa soka waliokuwa wakitazama laivu na wale waliotazama kupitia televisheni. Hawakuwa na presha, walitumia vipaji walivyojaaliwa na mbinu za walimu wao, kiasi cha kuufanya kuwa moja kati ya michezo ya kuvutia kuitazama dabi ya timu kubwa mbili za Simba na Yanga.
Mashabiki walivutiwa na soka lililopigwa kwa pande zote mbili, lakini hawakuvutiwa na baadhi ya maamuzi ya waamuzi, Elly Sasii wa Dar es Salaam, Mohamed Mkono kutoka Tanga, Kassim Mpanga kutoka Dar es Salaam, pamoja na Amina Kyando aliyekuwa mwamuzi wa akiba, akitokea Morogoro, huku mtathmini wao akiwa ni mwamuzi wa kimataifa wa zamani, Soud Abdi kutoka Arusha.
Tuseme tu pamoja na ubora wa mechi yenyewe, lakini haikutendewa haki na waamuzi, hasa Sasii aliyekuwa akionekana akichezesha kwa kutaka 'kutafuta uwiano wa matukio na si kufuata taratibu na sheria 17 za mchezo wa soka duniani.
Tumeshuhudia pande zote mbili zilikuwa zinalalamikia baadhi ya matukio ya mchezo huo, ambayo yalikuwa yakionekana dhahiri kwa refa aliyechezesha ama kwa kutojiamini au kwa woga.
Mara kwa mara tumekuwa tukiliongelea hili kuwa waamuzi wengi wa Tanzania wamekuwa hawajiamini na wamekuwa wakisita kutoa maamuzi magumu pale wanapotakiwa kufanya hivyo.
Haijulikana kama wanakuwa wanakwepa lawama, wanaogopa kuwa vichwa vya habari katika magazeti na simulizi kwenye mitandao ya kijamii au vipi.
Tuseme ukweli tu kuwa pamoja na kwamba soka la Tanzania limekua sana na kusifiwa na mataifa mbalimbali, huku Ligi Kuu ikitajwa kuwa ni ya sita kwa ubora barani Afrika, lakini imekuwa ikififishwa na maamuzi mengi yasiyo sahihi ya waamuzi.
Waamuzi ndiyo wamekuwa ni sumu ya mpira wa Tanzania kutokana na kufanya maamuzi mengi ya kushangaza na hata mara nyingine kuamua matokeo badala ya mchezo wenyewe.
Haiwezekani mtu anafanyiwa madhambi hatua tatu tu kutoka mwamuzi alipo, lakini anakataa kuwa si faulo.
Na hii yote inatokana na tabia ya kutaka kusawazisha kosa kwa kosa ambalo yeye mwenyewe ameliacha mwanzo.
Tunaweza kusema kama hali itakuwa hii, basi waamuzi wa Tanzania bado wana safari ndefu kuchaguliwa kuchezesha michezo mikubwa kama Fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON), ama michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika na Kombe la Shirikisho barani humu.
Kwa kilichotokea Alhamisi iliyopita, wala haishangazi kuona ni kwa nini waamuzi wetu hawateuliwi kuchezesha mashindano hayo ya Afrika.
Moja kati ya sifa za mwamuzi ni kujiamini na kuchukua maamuzi magumu kwa wakati sahihi, lakini wa kwetu hawapo hivyo.
Tuna wasiwasi hata Video ya Kumsaidia Mwamuzi (VAR), zinaweza zisiwe msaada sana kama hali hii itaendelea.
Huenda mwamuzi akaogopa hata kwenda kwenye video kuangalia marudio ili kufanya maamuzi sahihi.
Na hata akilazimishwa, anaweza kusimamia msimamo wake ule ule hata kama si sahihi kwa sababu pamoja na VAR kusaidia, lakini uamuzi wa mwisho huwa unabaki kwa mwamuzi mwenyewe.
Hapo ndipo tutakuja kugundua kuwa hata VAR yenyewe inaweza isiwe msaada kwetu kama tutaendelea kuwa na waamuzi wa aina hii.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED