Ulaji unaofaa utapunguza magonjwa yasiyoambukiza

Nipashe
Published at 10:06 AM Apr 19 2024
Ulaji unaofaa unapunguza magonjwa yasiyoambukiza.
PICHA: MAKTABA
Ulaji unaofaa unapunguza magonjwa yasiyoambukiza.

MAGONJWA yasiyoambukiza limekuwa tatizo kubwa kwa watanzania wengi kwasababu ya kutozingatia kanuni za afya ikiwamo ulaji unaofaa.

Kutokana na shughuli mbalimbali wanazojishughulisha, Watanzania wengi wanajikuta wanakula vyakula vya ovyo vinavyopikwa mitaani na hata vinavyopikwa majumbani havizingatii kanuni.

Idadi ya watu wanaoongezeka miili kwa kutozingatia ulaji unaofaa inasababisha kuibuka kwa magonjwa hayo yasiyoambukiza yakiwamo ya shinikizo la damu, moyo, kisukari na mengine.

Imeelezwa kuwa Mtanzania mmoja katika watatu ana uzito uliokithiri na watu wenye elimu na uhakika wa kipato wako kwenye kundi la waathirika zaidi.

Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Magonjwa yasiyoambukiza (NDC), katika Wizara ya Afya, Dk. Omary Ubuguyu, anaeleza katika maeneo machache ambayo Watanzania wanafanya vizuri ni kwenye mazoezi kwa sababu kumekuwa na mwamko mkubwa wa watu kukimbia, kutembea na mbio za marathoni nyingi.

Hata hivyo, inaelezwa katika masuala ya ulaji bado ni watu saba katika 100 ambao wanazingatia ulaji unaofaa.

Ukipita barabarani unaweza kukutana na mwanamke ukadhani ni mjamzito, lakini kumbe ana kiribatumbo kinachosababishwa na ulaji usiofaa au unywaji pombe uliopitiliza.

Inaelezwa kuwa suala la uzito na unene kupita kiasi hali imezidi kuwa mbaya, zamani ilikuwa ni katika kila watu wanne, mmoja ana uzito uliokithiri, sasa hivi ni mtu mmoja katika kila watu watatu ana uzito au unene uliokithiri.

Watalaamu wa afya wanaeleza kuwa vijana wanaathirika zaidi kuliko rika nyingine yoyote na wanawake wanaathirika zaidi kuliko wanaume katika ulaji usiofaa na unywaji pombe. Yaani watu wenye umri mdogo na wanawake ndio wako kwenye uhatarishi zaidi na inamaanisha kwamba jamii ipo katika hali ngumu sana. 

Utafiti unaonesha magonjwa yasiyoambukiza kama saratani, kisukari, figo na shinikizo la juu la damu, yanaathiri zaidi watu wenye kipato cha chini, lakini ni kinyume chake katika baadhi ya nchi kama Tanzania ambako waathirika wakubwa ni wasomi na wenye uhakika wa kipato.

Wafanyakazi ndio wanaotumia vyakula vya viwandani zaidi, pombe zaidi, ndio watu wenye fursa ya kununua soda na vitu vingine ambavyo vinaathiri afya.

Aidha, wafanyakazi wanaathirika zaidi kutokana na mtindo wa maisha kwa kuwa hawana nafasi ya kupata chakula bora kutokana na kununua vyakula wasivyojua namna vilivyoandaliwa na pia hawapati nafasi ya kufanya mazoezi.

Hali hii inasababisha taifa kuwa na mzigo mkubwa wa magonjwa yasiyoambukiza. Gharama katika matibabu kwa mfano Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), vitu vikubwa vinavyoelemea taifa ni kutibu magonjwa kama saratani, matatizo ya figo, shinikizo la juu la damu, kiharusi na kisukari. 

Njia ya kuondokana na tatizo hilo ni watu kujitahidi kufanya mazoezi kila siku, kula vyakula vyenye virutubisho, kupima afya mara kwa mara na kubadili mtindo wa maisha unaochochea magonjwa yasiyoambukiza.

Pia, waajiri wanapaswa kuhakikisha usalama mahala pa kazi na afya kuwa kipaumbele namba moja ili wafanyakazi waweze kufanya uzalishaji unaokusudiwa.

Mlo kamili unaopaswa kuzingatiwa kila siku na aina yake kwenye mabano ni wanga (ugali, wali au ndizi), mboga (kabichi, spinachi, mchicha au figiri), protini (nyama, samaki, kunde, njegere na maharage), matunda (embe, chungwa, papai au tikiti), vitamini (karanga au korosho) na maji ya kutosha.