TATIZO la watoto kuzaliwa na tatizo la vichwa vikubwa na mgongo wazi, linawakosesha raha wazazi wengi kutokana na kuwa na uwezo mdogo wa kugharamia matibabu ya watoto wao.
Wazazi wasiokuwa na uwezo hupoteza watoto wao kwa kukosa fedha za kuwagharamia kutokana na gharama zake kuwa kubwa.
Kwa wanaotembelea hospitali kubwa kama ya Muhimbili, unaweza kushuhudia kinamama wengi wakiwa wamepakata watoto wenye matatizo hayo huku wakiwa na nyuso za kukata tamaa.
Baadhi yao huokoa watoto wao kwa kuomba msaada kutoka kwa wasamaria wema au taasisi zinazotoa msaada wa matibabu hayo.
Kauli ya Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu kwamba Rais Samia Suluhu Hassan, atagharimia matibabu ya upasuaji kwa watoto 100 wenye vichwa vikubwa na mgongo wazi, imeleta faraja kubwa kwa wazazi ambao walishakata tamaa ya watoto wao kupona.
Matibabu hayo kwa mujibu wa Waziri wa Afya yatakayofanyika katika Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI).
Waziri Ummy alitembelea Taasisi ya Mifupa (MOI) kuwajulia hali watoto 25 waliofanyiwa upasuaji chini ya ufadhili wa MO Dewji Foundation.
Kutokana na tatizo hilo la watoto wenye vichwa vikubwa na mgongo wazi, Rais Samia ameguswa na ameamua kugharamia matibabu ya watoto hao ili kuepusha madhara na ulemavu unaoweza kusababishwa na kuchelewa kufanyiwa upasuaji.
Waziri Ummy alieleza kuwa amemsikia mwenyekiti wa chama cha wazazi na walezi wenye watoto wa tatizo hilo la kichwa kikubwa na mgongo wazi kwamba wana watoto kama 200 wanaopaswa kufanyiwa upasuaji, lakini wazazi hawana uwezo.
Akasema kuwa Rais Samia amemuelekeza, alete pesa kwa ajili ya watoto 100 ambao watafanyiwa upasuaji wa kichwa kikubwa na mgongo wazi bure.
Pia, akamuagiza Mkurugenzi wa Taasisi ya MOI kuwasiliana na chama hicho kuwabaini watoto wenye tatizo hilo ndani ya wiki moja na kuahidi kuwa wizara italeta hizo fedha.
Pamoja na jitihada za Rais Samia kusaidia watoto hao, ni vizuri pia wadau wengine wakajitokeza kusaidia juhudi hizo za Rais ili kuendelea kuokoa watoto wengi zaidi wenye tatizo hilo.
Kuna taasisi nyingi ambazo zinaweza kujitolea kwa kile wanachokipata kurudisha fadhila kwa jamii hasa kwenye matibabu kutokana na baadhi ya Watanzania kutokuwa na uwezo huo.
Kwa wazazi wenye watoto wenye tatizo hilo, wanapaswa kuwapeleka hospitali na kuachana na dhana kuwa wamelogwa na kuishia kwenda kwa waganga wa jadi ambao huwapa maelezo ya uongo na mwishowe kupoteza watoto wao.
Tatizo la vichwa vikubwa linaweza kuzuilika kwa kuhakikisha kinamama wanapokuwa wajawazito wanakula vyakula vyenye madini ya Frolic Acid na kuzingatia umuhimu wa kwenda kliniki.
Chama cha Wazazi na Walezi wa Watoto wenye vichwa vikubwa na mgongo wazi Tanzania (ASBATH), kimebainisha kuwa na orodha ya watoto 200 wanaohitaji matibabu, lakini kutokana na ukosefu wa fedha wameshindwa kupata matibabu hayo.
Idadi hiyo ni kubwa, lakini inaweza kuondolewa kwenye tatizo hilo kama Watanzania kwa umoja wao watajitoa kuwasaidia.
Kama watu wanaweza kuchangia mamilioni kwenye sherehe mbalimbali, kwanini kwenye matibabu ishindikane.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED