TIMU ya Soka ya Taifa maarufu Taifa Stars inatarajia kushuka dimbani leo ugenini kucheza dhidi ya Ethiopia.
Taifa Stars na Ethiopia zinakutana katika mechi ya kuwania tiketi ya kushiriki fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON 2025), fainali hizo zitachezwa mwakani nchini Morocco.
Timu hizo mbili ziko katika Kundi H, pamoja na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DR Congo) na Guinea.
Mechi nyingine ya kundi hilo itakayochezwa leo kuanzia saa 4:00 usiku itakuwa ni kati ya wenyeji Guinea dhidi ya DR Congo.
Tayari DR Congo yenye pointi 12 kibindoni imeshakata tiketi ya kucheza fainali hizo na katika msimamo wa kundi hilo inafuatiwa na Guinea yenye pointi sita, Taifa Stars ina pointi nne wakati Ethiopia inaburuza mkia ikiwa na pointi moja.
Kimahesabu, bila kujali au kufuatilia matokeo ya mechi nyingine, Stars inatakiwa kuvuna pointi sita katika mechi zake mbili zilizobakia.
Leo inatakiwa kuwafunga Ethiopia na baadaye kurejea nyumbani kuwasubiri Guinea na kuwachapa katika mchezo utakaofanyika Novemba 19, mwaka huu kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.
Katika siku za hivi karibuni, Stars imekuwa na matokeo chanya inapocheza ugenini na kuwa na wakati mgumu inapopambana kwenye ardhi ya nyumbani.
Hili linawezekana kubadilika endapo wachezaji watajituma kupata ushindi wa aina yoyote leo ugenini Kinshasa na baadaye kurejea kumaliza kazi hapa nyumbani kwa kuwafunga Guinea.
Ushindi katika mechi ya leo ni muhimu sana kwa Stars kwa sababu utawafanya wachezaji wawe kwenye morali ya juu kuelekea mchezo wa mwisho wa hatua hiyo ya makundi.
Katika soka hakuna kisichowezekana, kinachotakiwa ni kuwaamini wachezaji wetu ambao wameteuliwa na Kocha Mkuu, Hemed Suleiman 'Morocco' kupeperusha bendera ya Tanzania kwa sasa katika mashindano hayo.
Tunawakumbusha wadau wa soka nchini wakiongozwa na viongozi na wanachama wa klabu pendwa za Simba na Yanga, kuhamishia nguvu zile wanazowezeka pale wanapokuwa na mechi zao za dabi katika timu ya taifa kwa sababu tunahitaji kupata matokeo chanya.
Dua na kutoa mawazo chanya kuelekea mechi hizi mbili ndio jambo pekee ambalo tungependa kulisikia katika kipindi hiki kwa sababu tunataka kuwa na mwendelezo wa kushiriki mara kwa mara fainali za AFCON.
Kikubwa benchi la ufundi ambalo limepewa dhamana ya kuiongoza Stars inatakiwa kufanya kazi yake kwa kujiamini na kuwaambia wachezaji wetu wanaweza, hii itasaidia kuwaongezea nguvu, kila mchezaji atakayepata nafasi ya kucheza afahamu nchi inamtegemea, aingie uwanjani kupambana kwa ajili ya Watanzania wengine milioni 60 walioko nje.
Tunawakumbusha wachezaji wa Stars kufahamu hata mbuyu ulianza kama mchicha, mastaa ambao leo hii tunawaona katika klabu mbalimbali za Ulaya, walionekana kupitia mataifa yao na kufanya vyema kwa timu hiyo kutawatafanya wao na wengine wanaochipukia.
Kila mchezaji atakayevaa jezi ya Stars ajue yuko vitani na anatakiwa kupambana bila kukata tamaa, kufanya vizuri katika mechi ya leo, kutawarahisishia kukamilisha dakika nyingine 90 zilizobakia watakapoikaribisha Guinea.
Mungu ibariki Taifa Stars, Mungu ibariki Tanzania, nafasi ya kufuzu fainali za AFCON 2025 kwa nchi yetu tunayo.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED