KOCHA aliyeipa ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara kwa misimu mitatu mfululizo na msimu uliopita na kuifikisha hatua ya robo fainali ya mashindano ya kimataifa ya Ligi ya Mabingwa Afrika, Miguel Gamondi, ametimuliwa.
Gamondi alichukua mikoba ya Nasreddine Nabi, alikuwa mmoja wa makocha wenye misimamo, na aliitengeneza Yanga isiyokuwa na 'abiria' uwanjani.
Kwangu binafsi ni mmoja wa makocha ambao niliokuwa nawakubali kutokana na jinsi alivyoitengeneza Yanga kutomtegemea mchezaji mmoja.
Wakati wa Nabi, Yanga iliishi kwa kumtegemea, Fiston Mayele, ambapo wachezaji karibuni wengi wa Yanga wakimzunguka yeye kwa ajili ya kupata ushindi.
Hata mashabiki wa Yanga kama siku ambayo Mayele, aliyeuzwa katika klabu ya Pyramids ya Misri, hachezi, wanakuwa roho juu na hawana uhakika wa kupata ushindi.
Alipoichukua Gamondi alitengeneza mfumo ambao kila mchezaji alikuwa anamsaidia mwenzake.
Yanga ilikuwa ikikabia juu. Mastraika licha ya kufunga mabao walikuwa na kazi ya kuwafanya mabeki wa upinzani wasiwe huru na mipira.
Yanga ilikuwa inacheza mpira kwa kasi na hakukuwa na mfungaji mmoja. Si lazima straika akufunge.
Yeyote aliweza kufunga na kwa wakati wowote. Yanga iliogopeka siyo hapa nchini tu hata nje ya Tanzania.
Hiyo ndiyo Yanga na Gamondi, ambaye jana klabu hiyo ilitangaza rasmi kuachana naye.
Yote haya ni kutokana na vipigo viwili mfululizo vya bao 1-0 dhidi ya Azam FC na 3-1 dhidi ya Tabora United.
Hata hivyo yapo mengi yanazungumzwa na watu kutoka ndani ya Yanga kulikuwa na kutoelewana na viongozi kwa madai kuwa ni mbishi.
Mfano wengine wanasema hamtumii beki, Kibwana Shomari, kwa sababu zisizoeleweka na alifanya hivyo licha ya Yao Kouassi kuwa mgonjwa, aliamua kumtumia, Denis Nkane, ambaye si eneo lake.
Wanaomtetea kocha huyo nao wamedai Gamondi alianza kuingia kinyongo katika usajili wa dirisha kubwa, baada ya kuletewa wachezaji ambao hawakuwa chaguo lake.
Wachezaji hao ni Clatous Chama na Jean Baleke, huku mwenyewe akielekeza wasajiliwe wachezaji ambao hawakusajiliwa.
Binafsi hadi sasa sijaona sababu hasa ya viongozi wa Yanga kumtimua kocha huyo. Na ndiyo sababu hata uongozi haujasema sababu hasa ya kuchukua uamuzi huo. Sidhani kama tatizo la kutofanya vyema katika michezo miwili ya Ligi Kuu ndio msingi wa Gamondi kutemwa.
Ukiangalia tangu kuanza kwa msimu huu, Yanga imepoteza ule uchezaji wake uliozoeleka na ilionekana iko karibu kupoteza mechi kuliko kushinda, kila ilipokuwa ikicheza mchezo mmoja.
Na kupoteza mechi mbili kumechangiwa mno na makosa ya kibinadamu ya waamuzi, la sivyo ingekuwa imepoteza mechi nyingi zaidi ya hizo mbili.
Ninavyoona mimi tatizo lipo kwa wachezaji wa Yanga ambao walikuwa kwenye kiwango cha juu msimu uliopita, lakini msimu huu kimepungua.
Wachezaji kama Stephane Aziz Ki, Pacome Zouzoua, Clement Mzize, Kennedy Musonda na wengine waliokuwa mhimili wa Yanga, msimu huu hawajaanza wakiwa na makali yao.
Imedaiwa pia baadhi ya wachezaji wa timu hiyo wamevimba 'vichwa' kutokana na umaarufu, hivyo kujiingiza katika starehe, hali inayosababisha viwango vya vipungue.
Mimi nadhani viongozi wa Yanga, wangemsaidia kocha kwa kusajili wachezaji ambao wangekuja kuisukuma hapo ilipo kwenda mbele.
Viongozi wa Yanga wangeanza kuangalia kuwaondoa baadhi ya wachezaji ambao wamekuwa na majina makubwa lakini mchango wao kwa sasa ni mdogo na kusajili wengine kama walivyofanya watani zao wa jadi Simba, badala ya kumtimua Gamondi.
Nina uhakika kama Gamondi angepata wachezaji wenye umri mdogo kama wale waliopo Simba, angeitengeneza Yanga ambayo ingekuwa na kasi zaidi kuliko hata hii tuliyoiona msimu uliopita.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED