Kimya cha viongozi Simba hakina afya kwa mashabiki

Nipashe
Published at 01:16 PM Apr 22 2024
Meneja wa habari wa Klabu ya Simba, Ahmed Ally.
PICHA: SIMBA SC
Meneja wa habari wa Klabu ya Simba, Ahmed Ally.

WANACHAMA na mashabiki wa Simba wanapitia katika wakati mgumu kutokana na timu yao kutofanya vizuri kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu, hivyo kuelekea kuukosa ubingwa huo kwa msimu wa tatu mfululizo.

Lakini pia katika michuano ya kimataifa, imetinga hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa kwa mbinde kabla ya kuondoshwa na Al Ahly ya Misri na kushindwa kufikia lengo lao la kufika nusu fainali ya mashindano hayo.

Kadhalika, msimu huu imefungwa na watani zao wa jadi, Yanga nyumbani na ugenini, ikianza kukubali kipigo cha mabao 5-1 Novemba 5, mwaka jana, kabla ya juzi kufungwa 2-1.

Baadhi ya mashabiki na wanachama wa klabu hiyo walianza kwa kunung'unika kuwa timu yao kila muda unavyozidi kwenda badala ya kuimarika inazidi kuporomoka, ambapo walihoji tatizo ni nini? Lakini hawakujibiwa.

Wengine wakitoa maoni yao kuhusu mwenendo mbaya wa timu yao, lakini wakaitwa wachochezi.

Kwa sasa kikosi cha Simba kinaonekana kwenda, 'Mungu nisaidie', kwani msimu huu hakijawa na kiwango ambacho Wanamsimbazi wenyewe wamekizoea na wengi wanaamini kuwa usajili mbovu usiokuwa na malengo unaofanywa na baadhi ya viongozi ndiyo ulioifikisha timu yao hapo ilipo.

Hilo linadhihirishwa pia na  matokeo ya hivi karibuni ya timu hiyo ambapo imetolewa kwenye hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika, ikichapwa bao 1-0 nyumbani na mabao 2-0, ugenini dhidi ya Al Ahly, hiyo ikiwa ni mara ya kwanza kwa timu hiyo kupata matokeo dhidi ya Simba hapa nchini.

Kama vile haitoshi, ikatolewa kwenye hatua ya 16-bora ya Kombe la FA kwa mikwaju penalti 6-5 dhidi ya Mashujaa FC, na hata iliporejea kwenye mechi za Ligi Kuu, ikakwaa kigingi cha sare ya bao 1-1 dhidi ya Ihefu FC.

Mpaka hapo tu, inaonyesha namna mashabiki wa Simba hali yao ilivyo, na wamekuwa wakilalamika, lakini hakuna kiongozi hata mmoja wa klabu hiyo aliyejitokeza na kuwaambia hali halisi ilivyo.

Mtu pekee ambaye anaonekana ni kiunganishi cha klabu, wanachama na mashabiki ni, Meneja Habari na Mawasiliano, Ahmed Ally, ambaye naye baada ya kipigo cha juzi, hajaongea chochote.

Viongozi wao waliowachagua na walioteuliwa wapo kimya, kama vile hakuna kinachotokea. Hali hii si nzuri hasa ikizingatiwa kuwa viongozi hao wako hapo kwa ajili ya hao hao wanachama na mashabiki.

Klabu ni kama kampuni, ama tasisi na wanachama na mashabiki ni kama wateja wa bidhaa zinazozaliswa, hawa ndiyo wanaokata tiketi kuingia viwanjani, kununua skafu, jezi na vitu vingine, hivyo kuwaacha bila kuwaambia kitu chochote ni kutowatendea haki.

Ni wajibu wa baba, mama au mzazi kuongea chochote kile pale familia inapopitia kwenye hali ngumu, ili kuwapa faraja, na matumaini hata kama hayapo. Mlezi ndiye ana dhima ya kumbembeleza mtoto anapokabiliana na hali ngumu na ya kukatisha tamaa, hivyo viongozi wa Simba hawana budi kufanya hivyo.

Tunaamini kukaa kimya namna hiyo hakuleti afya kwa maendeleo ya klabu yao, kwani viongozi hao hawataeleweka kama wakijitokeza wakati mwingine wowote, kwa kuwa kiongozi mzuri ni yule anayeongoza na kuwa na watu wake wakati wa raha na shida.

Simba ni taasisi kubwa kwa sasa kutokana na kuwa na wafuasi wengi, hilo viongozi wanapaswa kulitambua, bila hawa wanaolia na kulalamika kwa sasa hata wao wasingejivunia kuongoza klabu hiyo.

Wanachama na mashabiki wa Simba wanapaswa kuelezwe kila kitu kuhusu mwenendo wa klabu yao, ili kuilinda 'brand' klabu kimya hiki cha viongozi kinaweza kuishusha zaidi.