Imeelezwa kwamba hali ya amani, utulivu, na ushirikiano unaosimamiwa na viongozi wakuu wa nchi imesaidia kuleta chachu kubwa ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo Tanzania Bara na Tanzania Visiwani.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, na Uratibu), William Lukuvi, alitoa kauli hiyo jana Januari 08, 2025 wakati wa hafla ya uwekaji wa jiwe la msingi katika ujenzi wa jengo jipya la Mahakama ya Wilaya ya Mkoani. Hafla hiyo ilikuwa sehemu ya Maadhimisho ya Miaka 61 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar ya mwaka 1964.
Akizungumza katika hafla hiyo, Lukuvi alisisitiza umuhimu wa kuendelea kuwaombea viongozi wa nchi kwa dini zetu mbalimbali ili Mwenyezi Mungu awape afya na nguvu za kuendelea kuongoza kwa mshikamano. Alibainisha kuwa, "Chini ya uongozi wao, Tanzania Bara na Tanzania Visiwani zimetulia, hali ambayo imewezesha utekelezaji wa miradi mikubwa ya maendeleo. Mwenye macho haambiwi tazama."
Waziri Lukuvi aliongeza kuwa maendeleo makubwa yanayoendelea kutekelezwa na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar chini ya uongozi wa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi, ni jambo la kujivunia. Alieleza kwamba mafanikio ya Serikali ya Awamu ya Nane yanaonekana wazi katika nyanja za siasa, utawala bora, uchumi, huduma za kijamii, na utamaduni wa watu wa Visiwa vya Zanzibar.
Akifafanua zaidi, Waziri Lukuvi alisema Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imechukua hatua madhubuti kwa kuanzisha mradi wa ujenzi wa majengo saba ya Mahakama za Wilaya na Mikoa. Hatua hiyo inalenga kukabiliana na changamoto za miundombinu ya majengo ya mahakama na kuimarisha utoaji wa huduma kwa wananchi. Ujenzi wa jengo la Mahakama ya Wilaya ya Mkoani ni sehemu ya utekelezaji wa mradi huo, ambao ulipangwa kufanyika katika mwaka wa fedha 2023/2024.
Kwa upande wake, Jaji Mkuu wa Zanzibar,Khamis Ramadhan Abdalla, alielezea shukrani zake kwa Rais Dk. Hussein Ali Mwinyi kwa juhudi za kuhakikisha upatikanaji wa miundombinu bora ya mahakama. "Tumekusudia kusogeza huduma kwa wananchi kwa kujenga mifumo imara ya usimamizi wa haki ili kuboresha huduma zetu za mahakama kuwa za kisasa," alisema Jaji Abdalla.
Naye Mrajis wa Mahakama Kuu Zanzibar, Valentina Katema, alibainisha kuwa miundombinu ya sasa ya mahakama ipo katika hali ya zamani, hali inayosababisha changamoto katika uendeshaji wa shughuli za mahakama. Alisema, "Ujenzi wa majengo mapya ya mahakama utasaidia kupunguza msongamano wa huduma, kuboresha mazingira ya kazi, na kuendana na mahitaji ya kisasa."
Hafla hiyo ilihitimishwa kwa matumaini makubwa kuwa miradi ya ujenzi wa miundombinu ya mahakama itachangia kuboresha usimamizi wa haki na kuimarisha utoaji wa huduma bora kwa wananchi wa Zanzibar na Tanzania kwa ujumla.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED