Ratiba kombe la Muungano iwe katika kalenda maalum

Nipashe
Published at 06:32 AM Apr 27 2024
Nembo za Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania na Shirikisho la Mpira wa miguu Zanzibar.
Picha: Mtandaoni.
Nembo za Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania na Shirikisho la Mpira wa miguu Zanzibar.

MASHINDANO ya kuwania Kombe la Muungano ambayo hushirikisha timu zilizofanya vizuri kutoka Tanzania Bara na Visiwani Zanzibar yamerejea rasmi mwaka huu.

Mashindano hayo ambayo miaka ya nyuma yalitoa wawakilishi wa Tanzania katika michuano ya kimataifa inayoandaliwa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF), yalikuwa hayajafanyika kwa kipindi cha miaka 20.

Kesho ndio mechi ya fainali ya mashindano hayo kwa mwaka huu itachezwa kati ya Simba dhidi ya mshindi kati ya Azam na KMKM. Simba imetinga fainali baada ya kuifunga KVZ ya Zanzibar mabao 2-0.

Hata hivyo kutokana na ratiba kuwa finyu, michuano ya mwaka huu imeanzia hatua ya nusu fainali.

Badala ya kufanyika kama ilivyozoeleka miaka ya nyuma ambayo ilishirikisha timu nane, nne kutoka kila upande na mashindano hayo kuonekana kuwa na ushindani, lakini kila timu ilijiandaa vyema kuhakikisha inabeba ubingwa na wakati huo huo inapata tiketi ya kushiriki mashindano ya kimataifa lakini pia kujenga heshima.

Zanzibar kupata uanachama CAF na timu zake kupata tiketi ya kushiriki mashindano ya kimataifa ya Ligi ya Mabingwa Afrika na Kombe la Shirikisho Afrika, ni moja ya sababu zilizopelekea kufutwa au kutofanyika kwa michuano hiyo, lakini pia migogoro kati ya waliokuwa viongozi wa Chama cha Soka Tanzania (FAT sasa TFF) na wenzao wa Zanzibar (ZFA sasa ZFF), pia kulichangia 'kuua' mashindano ya Kombe la Muungano.

Udhamini kutoka katika makampuni yanayozalisha vinywaji vya pombe ambayo hayakuwa yakiruhusiwa kudhamini timu au mashindano huko Zanzibar ni sababu  nyingine iliyofanya pia michuano hiyo 'kuzikwa' hapa nchini.

Kama vile imeonekana mashindano ya mwaka huu yamekuwa ya zima moto, inadaiwa mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Yanga wamejitoa katika michuano hiyo kwa sababu ambazo hawakutaka kuziweka wazi.

Taarifa zaidi zinadai Yanga imejitoa kwa sababu haitaki kuharibu 'furaha' yake ya kumfunga mtani wake Simba, baada ya kumfunga michezo yote ya Ligi Kuu msimu huu, maana ndani ya siku chache, timu hizo mbili zingeweza kukutana katika fainali ya Kombe la Muungano, hivyo Yanga 'imechomoa' kushiriki na imeweka wazi sasa inaweka nguvu zake katika kuhakikisha inatetea ubingwa wa Bara wanaoushikilia.

Na katika kuonyesha mashindano hayo ya Kombe la Muungano kwa mwaka huu hayakuwa katika ratiba rasmi kwenye msimu wa mwaka 2023/2024, imelazimika Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB), kuahirisha mechi kati ya Simba dhidi ya Dodoma Jiji iliyopaswa kuchezwa Aprili 23, mwaka huu na sasa kupangiwa siku nyingine, ili kuruhusu kikosi cha Wekundu wa Msimbazi kwenda Zanzibar kushiriki michuano hiyo.

Ni ngumu kusema michuano hiyo ya mwaka huu ilikuwa katika kalenda ya mashindano na endapo Simba na Yanga zingefanikiwa kutinga hatua ya nusu fainali ya mashindano ya kimataifa ya Ligi ya Mabingwa Afrika, je michuano hiyo ingekuwepo?

Umefika wakati kwa Kamati ya Mashindano ya TFF na ZFF kukaa pamoja na kupanga kalenda rafiki ambayo itawezesha michuano hiyo kufanyika kila mwaka na kanuni zake zikawekwa hadharani.

Kwa kufanya hivyo, mashindano ya Kombe la Muungano yatarejesha heshima yake na kufanya timu zitakazofuzu kujipanga kuonyesha ubora wake na yasirejee tena  kwa kushtukiza kama yalivyofanyika mwaka huu.

Na katika kuhakikisha yanafanyika katika kuendeleza soka na mshikamano wa pande hizi mbili za Tanzania, kwa maana halisi ya kudumisha Muungano, pia yaandaliwe mashindano yatakayohusisha na timu za wanawake, ambayo yanaweza kusaidia wachezaji kupata maandalizi kuelekea michuano ya kimataifa ya Afrika Mashariki na Kati.