Wananchi msiweke rehani maisha mvua inaendelea

Nipashe
Published at 10:23 AM Apr 24 2024
Mvua.
PICHA: MAKTABA
Mvua.

MVUA ya masika inaendelea kunyesha maeneo mbalimbali nchini na kuleta athari kubwa ya mafuriko huku wengine wakipoteza makazi na mali.

Kabla mvua hii haijaanza kunyesha Mamlaka ya Hali ya Hewa (TMA), ilitoa tahadhari kwa wananchi wanaoishi maeneo hatarishi kuondoka mapema ili kujiepusha na madhara.

Mabadiliko ya tabia nchi yamesababisha nchi nyingi duniani kuathirika na mvua na hata nchi zilizoendelea zenye miundombinu mizuri pia zimeathirika na mafuriko.

Katika mitandao ya kijamii kuna picha za video zinazoonesha baadhi ya nchi hizo zikipitia wakati mgumu baada ya nyumba kuzingirwa na maji huku barabara zikiwa zimejaa maji mithili ya mito.

Hii inasababishwa na mabadiliko hayo ni hali ambayo haiwezi kunyoosheana vidole.

Hatahivyo, athari hizo zimekuwa zikijadiliwa kote duniani na cha muhimu ni kuendelea kuchukua tahadhari ili binadamu na mali zao zisiendelee kuangamia.

Kuna nchi ambazo maisha ya watu yamepotea kwa kusombwa na maji na vile vile, mali ikiwamo magari yakisombwa na mafuriko hayo.

Kwa nchi zinazoendelea kama Tanzania, athari hizo zinaweza kuepukika kama wanaoishi kwenye maeneo hatarishi wataondoka na kutafuta sehemu nyingine zenye usalama zaidi.

Kuna umuhimu pia wa kuimarisha miundombinu ya barabara ikiwamo mitaro inayopitisha maji kutunzwa ili uchafu usitupwe ndani kuruhusu maji yanapokuwa mengi kupita bila tatizo.

Hata hivyo, kumejitokeza tabia kwa baadhi ya watu kuendelea kuharibu miundombinu hiyo kwa kutupa taka na kusababisha maji kupita na kwenda baharini.

Hili la utupaji taka kwenye mitaro linasababishwa pia na kutozingatia usafi wa mazingira hasa uzoaji taka kwenye mitaa na maeneo ya watu wanayofanyia biashara hasa pembezoni mwa barabara.

Mitaani nyumba nyingi zimejitahidi kukusanya taka na kuzihifadhi kwenye mifuko, lakini magari ya kusomba taka hizo hayajaonekana kwa muda mrefu na matokeo yake taka hizo zinajaa na kuanza kuchafua mazingira.

Kuna wananchi ambao wanaishi kwenye mazingira hatarishi ambayo kila mvua inaponyesha nyumba zao zinazingirwa na mafuriko, lakini wako radhi kuishi kwenye adha hiyo kwa madai kuwa mvua itapita na maisha yataendelea kama kawaida.

Wengine wanagoma kuishi kwenye maeneo hayo hatarishi wakidai kuwa ni karibu na mjini ambako sehemu za shughuli za kujipatia kipato zinafikika bila kuhitaji kutumia nauli kupanda usafiri wa umma.

Watu hao hao, huwa wa kwanza kulalamika pale mafuriko yanapoharibu nyumba na mali zao na kuilaumu serikali kuwa haiwajali.

Baadhi ya watu wameamua kuweka rehani maisha yao kwa kuamini kuwa mvua itanyesha mara moja na kuondoka zake, mpaka itakaponyesha wakati mwingine wao watakuwa wamerudi kwenye maisha yao ya kawaida.

Kwa mujibu wa TMA mvua hii ya masika itanyesha katika mikoa mingi nchini na wananchi wametakiwa kuchukua tahadhari ya hali ya juu ili wasiweze kudhurika.

Maeneo yaliyoanza kuathiriwa na mvua hiyo yameonekana ikiwamo Rufiji ambako nyumba nyingi zimefunikwa na maji na watu kufa maji baada ya kusombwa na mafuriko.

Tumaini la kupata mavuno limeondoka baada ya mazao yao kusombwa na kinachohitajika ni msaada kunusuru ndugu zetu.