Ujumbe wa viongozi wa dini utiliwe maanani

Nipashe
Published at 11:03 AM Apr 09 2024
Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Askofu Dk. Alex Malasusa.
PICHA: MAKTABA
Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Askofu Dk. Alex Malasusa.

WAKATI wa maadhimisho ya Sikukuu ya Pasaka (kumbukumbu ya kufufuka kwa Yesu Kristo), viongozi mbalimbali wa madhehebu ya dini ya kikristo pamoja na viongozi wa kiserikali, walitoa ujumbe mzito kuhusu maadili ambao hauna budi kufanyiwa kazi ili kuepusha kuendelea kuona maadili hayo yakiporomoka siku hadi siku.

Mambo makuu yaliyozungumzwa na viongozi hao ni kuhusu vitendo vya rushwa kushamiri katika maeneo muhimu ambayo wananchi ni kimbilio lao na kutegemea kupata haki zao, ukatili dhidi ya watu wengine, ambao kwa miaka ya hivi karibuni kumeshuhudiwa vitendo vingi vya mauaji au kufanyiana vitendo vya kinyama na vile vile mapenzi ya jinsia moja kuingia kwa kasi.

Kushamiri kwa kuporomoka kwa maadili sio dalili nzuri hivyo kuna kila sababu viongozi wakiwamo wa dini kulizungumzia ili watu warudi kwenye imani zao na kumwogopa Mungu.

Vitendo vya rushwa vimekuwa vikikwamisha mambo mengi na wakati mwingine kusababisha dhuluma kwa watu wanaostahili kuwa na haki ya kumiliki mali au kupata haki.

Mauaji au vitendo vya kinyama baadhi chanzo chake kinatokana na rushwa. Mtu anayestahiki kupata haki anadhulumiwa na kutokana na uonevu huo, aliyedhulumiwa anaamua kufanya jambo lolote ikiwamo kuua ili wote wakose.

Suala la maslahi duni pia linasababisha baadhi ya watumishi wa umma na wanaofanyakazi kwenye sekta binafsi kutumia mbinu nyingine ya kujiongezea kipato na matokeo yake kujiingiza kwenye vitendo vya rushwa na kuendelea kuota mizizi.

Rushwa ni tatizo kubwa kiasi cha kusababisha hata mtu anapopatiwa huduma anayostahili anaona kama amependelewa na kuamua kutoa pesa kuonyesha shukrani.

Mauaji katika jamii yanayosababishwa na wivu wa mapenzi, yameshamiri na hii inatokana na walio kwenye mahusiano kushindwa kuaminiana kutokana na kutomtanguliza Mungu mbele.

Hata watoto wasio na hatia wanaingizwa kwenye unyama huu kwa sababu tu wazazi wameshindwa kuelewana na wao kuwa waathirika.

Suala la mapenzi ya jinsia moja ni tishio kwa vijana wengi na hiyo inatokana na tamaa ya kuishi maisha wasiyokuwa na uwezo nayo na vilevile kuiga utamaduni wa nchi za kimagharibi.

Vijana wengi wanaangamia kwa sababu hawataki kufanyakazi, lakini wanataka kuishi maisha ya hali ya juu ya kuendesha magari mazuri na kuishi kwenye nyumba za kifahari na kuvaa mavazi ya gharama.

Wengi huishia kulelewa na wanawake watu wazima walio umri sawa na mama zao na wengine kutumbukia kwenye mapenzi ya jinsia moja.

Kijana wa kiume anaonekana ana nguvu za kutosha kufanyakazi na kupata kile anachokitaka, lakini hataki kufanyakazi na badala yake anaishia kujiremba kama mtoto wa kike kwa kuvaa hereni na kujichubua ngozi ili aonekane na mvuto.

Hali hiyo haithiri vijana wa kiume pekee, hata kwa vijana wa kike wapo wanaopendana na kuoana wenyewe kwa wenyewe.

Hii inafikirisha kwa kuwa kama vijana hao ndio tegemeo la taifa la baadaye halafu wanaachwa wakiangamia, tutakuwa na taifa la namna gani.

Kauli za viongozi wa dini ni lazima zifanyiwe kazi ili kuepusha vijana wengi kuendelea kuangamia. Wazazi wana jukumu kubwa la kufuatilia watoto wao nyendo zao badala ya kuwaachia jukumu hilo walimu au wasaidizi wa nyumbani.