MAPEMA mwaka huu, Watanzania walipata adha ya kupanda kwa bei ya sukari. Licha ya kupanda bei, bidhaa hiyo ilikuwa adimu kupatikana kutokana na kuuzwa kwa kificho na hata ilipopatikana, iliuzwa kwa bei kubwa hadi Sh. 8,000 kwa kilo.
Kutokana na kupanda huko, serikali ilifanya kila jitihada kuhakikisha wananchi wanaondokana na adha hiyo kwa kuchukua hatua mbalimbali ikiwamo kutoa vibali kwa ajili ya kuagiza nje ya nchi kuziba pengo lililokuwapo.
Jana, Rais Samia alivunja ukimya kuhusu adha hiyo kwa kubainisha kuwa alipata maumivu baada ya kusikia bidhaa hiyo ambayo ni muhimu kwa maisha ya kila siku ya mwanadamu na viwandani, ikiuzwa kwa bei hiyo takriban mara mbili na nusu ya bei iliyokuwapo awali.
Rais alibainisha kuwa uhaba huo wa sukari ulisababishwa na viwanda vya kuzalisha bidhaa hiyo, kushindwa kufanya uzalishaji kutokana na mvua nyingi zilizonyesha kuanzia Januari hadi Aprili, mwaka huu.
Habari njema ni kwamba Rais ameliona hilo na katika kuonesha dhamira ya kweli kwa wananchi kutokupata adha kwa wakati ujao, ameagiza upanuzi wa kiwanda cha pili cha sukari ya Mkulazi (Mkulazi II) baada ya kile cha awamu ya kwanza, mkoani Morogoro, kilichozinduliwa jana kikiwa kimekamilika kwa kugharimu Sh. bilioni 340. Kiwanda hicho kinamilikiwa kwa ubia kati ya Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) na Jeshi la Magereza.
Rais Samia, wakati wa uzinduzi huo, aliagiza kuanza kwa ujenzi wa kiwanda kipya cha Mkulazi II ili taifa liwe na uhakika wa chakula hasa sukari baada ya kukamilika na kuanza uzalishaji wa tani 50,000 kwa mwaka kwa Mkulazi I kilichoko Mbigiri, Kilosa mkoani Morogoro.
Rais alisema baada ya kukamilika kwa kiwanda hicho cha pili, uzalishaji wa sukari kwa Mkulazi I na Mkulazi II utafikia tani 70,000 kutoka 50,000 zinazozalishwa sasa, hatua ambayo itawezesha kupunguza pengo kubwa la bidhaa hiyo. Licha ya kuongeza uzalishaji na kuziba pengo la uhaba, Rais Samia alisema hakutakuwa na visingizio vya upungufu wa sukari mvua ikinyesha kwa kuwa viwanda hivyo vya serikali vitakuwa vikiendelea na uzalishaji.
Kwa ujumla, hatua hiyo ya serikali ya kuongeza kiwanda kingine cha sukari, ni ya kupongezwa kwa sababu imeona kwa kina wananchi waliopata adha wakati bidhaa hiyo ilipoadimika na kununua bei ya kuruka. Vioja hivyo vya wafanyabiashara vya kuficha sukari kila kunapokuwa na uzalishaji kidogo vitafikia tamati.
Licha ya hiyo, viwanda hivyo vitawezesha kupatikana kwa ajira kwa vijana ambao kilio hicho kimekuwapo muda mrefu na hata kuonekana sawa na donda ndugu lisilipata tiba mujarabu.
Pamoja na pongezi hizo, ni wakati mwafaka kwa serikali kujifunza kuhusu kuporomoka na kufa kwa viwanda na mashirika ya umma kulikosababisha wafanyakazi wengi kupunguzwa kazi na wengine kukosa stahiki zao.
Katika kujifunza huko, serikali inapaswa kujiondoa kwenye uendeshaji wa kila siku wa viwanda hivyo na kuweka menejimenti yenye uwezo na itakayooongoza taasisi kwa ufanisi na weledi. Serikali kazi yake inapaswa kuwa na bodi imara ya wakurugenzi itakayosimamia sera na miongozi katika utekelezaji wa majukumu ya kila siku.
Ni dhahiri kwamba kama ilivyo kwa msemo kwamba usiangalie ulipoangukia bali ulipojikwaa. Serikali itafanya hivyo kwa ustawi wa viwanda hivyo vya sukari na hatimaye kuleta tija na kuwaondolea Watanzania adha ya ukosefu wa sukari.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED