Serikali ilipe wazabuni wake kwa wakati kuepuka hasara

Nipashe
Published at 12:12 PM Jun 21 2024
CAG mstaafu Utouh.
Picha: Mpigapicha Wetu
CAG mstaafu Utouh.

Katika toleo letu la jana, tulikuwa na habari kuhusu serikali kuuziwa bidhaa na huduma kwa bei kubwa kuliko iliyoko sokoni.

Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali (CAG) wa zamani, Ludovick Utouh alisema hali hiyo inachangiwa na tabia iliyoko serikalini ya kuchelewesha malipo kwa wazabuni. 

Kwa mujibu wa Utouh, hivi sasa Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya WAJIBU, wazabuni hulazimika kuweka bei kubwa kuliko ya bei ya sokoni wanapoomba zabuni serikalini kwa kuwa serikali hawana uhakika wa kulipwa kwa wakati. 

Utouh aliyekuwa CAG nchini kwa miaka minane kuanzia 2006 hadi 2014, alisema kuwa mzabuni hulazimika kuiuzia serikali bidhaa au huduma kwa bei kubwa ili kulinda thamani ya fedha pale malipo yake yatakapocheleweshwa. 

Kukiwa na angalizo hilo la CAG mstaafu, Januari 30, mwaka huu, Waziri wa Fedha, Dk. Mwigulu Nchemba alitoa taarifa bungeni kuwa katika kipindi cha kuanzia mwaka wa fedha 2016/17 hadi Desemba 2023, serikali ililipa wazabuni na makandarasi wa ndani zaidi ya Sh. trilioni 2.1 kati ya madai ya zaidi ya Sh. trilioni 3.1 yaliyowasilishwa. 

Alisema kuwa madeni ya Sh. bilioni 981.79 yalikataliwa kutokana na sababu mbalimbali, ikiwamo kukosekana kwa nyaraka, madeni kubainika kulipwa tayari pamoja na makosa ya ukokotoaji. 

Kwa mujibu wa waziri huyo, serikali imeongeza bajeti ya kulipa madeni kutoka wastani wa Sh. bilioni 400 hadi Sh. bilioni 700 kwa mwaka na kuahidi kuwa  madai ya wazabuni na makandarasi yataendelea kulipwa kadri watakavyowasilisha hati zao za kukamilisha kazi. 

Hata hivyo, Nipashe tunafahamu kwamba ucheleweshaji malipo ya wazabuni na makandarasi unakiuka sheria za nchi. Kifungu cha 44(1) cha Kanuni za Ununuzi wa Umma za Mwaka 2013 kinaelekeza kwamba, ili kuzisaidia kampuni za ndani na kuziwezesha kutekeleza majukumu yao ya mkataba, taasisi nunuzi lazima zihakikishe malipo yanafanyika kwa wakati kwa wazabuni.  

Vilevile, inaporejewa Ripoti ya CAG kwa Mwaka 2022/23, inaeleza kuwa baada ya kukagua na kuthibitisha taarifa za kifedha za wizara, idara

zinazojitegemea, na wakala za serikali, alibaini kuwapo madeni ambayo hayakulipwa yenye thamani ya Sh. trilioni 3.39 kufikia tarehe 30 Juni 2023 katika taasisi 20. 

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, kati ya fedha hizo, Sh. bilioni 228.16 (asilimia saba) zilikuwa madai ya wafanyakazi; Sh. trilioni 1.37 (asilimia 40) zilikuwa madeni ya wazabuni; na Sh. trilioni 1.79 (asilimia 53) zilikuwa madeni mengine.  

Madeni yenye thamani ya Sh. trilioni 1.88 (asilimia 56 ya madeni yote) ni ya muda mrefu, yakiwa yamelimbikizwa kwa zaidi ya miezi 12 na madeni yenye thamani ya Sh. trilioni 1.51 (asilimia 44) ni ya kipindi cha chini ya miezi 12.  

Ni takwimu zinaonesha kuwapo umuhimu wa kuweka jitihada zaidi ili kuzuia madeni ya aina hii kuongezeka zaidi serikalini na kuchochea wazabuni kuizuia bidhaa na huduma serikali kwa bei kubwa zaidi ya soko kama ilivyofafanuliwa na CAG mstaafu Utouh. 

Tukitambua athari za wazabuni kuizuia serikali huduma na bidhaa kwa bei ghali, tunashauri taasisi nunuzi kulipa wazabuni na makandarasi kwa wakati. Utaratibu uliopo unaongeza mzigo kwa serikali - malipo ya ziada kwa wazabuni yangetumika kutekeleza miradi au kutoa huduma muhimu kwa wananchi. 

Tunakumbusha pia taasisi za serikali kuwa Kanuni E. 23 ya Kanuni za Kudumu za Utumishi wa Umma za Mwaka 2009 inataka madai ya wafanyakazi kulipwa wakati yanapojitokeza. 

Hivyo, ni muhimu serikali (Wizara ya Fedha) na taasisi nunuzi watoe kipaumbele katika utoaji fedha kwa ajili ya kulipa madeni ili kupunguza hatari zinazoweza kutokea kwa kuchelewesha malipo, ikiwamo wazabuni kuizuia serikali huduma kwa bei ghali zaidi ya soko.