MAKAMU Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Tundu Lissu, amesimama mahakamani kama wakili kutetea kesi katika Mahakama ya Wilaya ya Singida ikiwa ni miaka saba tangu aliposhambuliwa kwa risasi jijini Dodoma, Septemba 7, 2017.
Wakili Lissu alisimama jana mahakamani kutetea kesi ya jinai inayomkabili Askofu Mwanamapinduzi Machumu Kadutu ambaye amefunguliwa kesi ya jinai katika Mahakama ya Wilaya ya Singida.
Akizungumza na waandishi wa habari katika viwanja vya mahakama baada ya kutoka mahakamani, Wakili Lissu alisema kuwa baada ya kurejea katika kazi ya uwakili kama yangekuwa mapenzi yake, asingependa kusimamia kesi alizodai "za uonevu na hazina kichwa wala miguu" wanazofunguliwa watu.
"Kama ingekuwa mapenzi yangu nisiwe ninasimamia hizo kesi, nisiwe ninasimamia watu kwa kesi za uonevu, kama ingekuwa mapenzi yangu watu waache kuonewa, kufunguliwa kesi zisizokuwa na kichwa wala miguu ili mimi nifanye kazi nyingine, kwani muda wangu ni mfupi," alisema.
Wakili Lissu alidai kesi hiyo imeahirishwa hadi Oktoba 28 mwaka huu kwa kuwa Hakimu Mfawidhi anayeisimamia hakuwapo.
"Nimesafiri kutoka Dar es Salaam ili kuja (katika kesi) kuambiwa hakimu hayupo. Nilifikiri katika zama hizi za teknolojia tungeweza kupata taarifa katika simu kwamba, Hakimu Mkazi hayupo badala ya kuingiza watu gharama kusafiri hadi Singida," alidai.
Kwa mujibu wa maelezo yaliyoko katika hati ya mashtaka, ni kwamba Juni 3 mwaka huu, katika viwanja vya soko la zamani eneo la madukani kijiji cha Ibaga, wilayani Mkalama, mkoani Singida, Kadutu wakati akiwahutubia wananchi katika mkutano wa kisiasa, inadaiwa alichochea wakazi wa Ibada.
Katika hati ya mashtaka, maneno hayo ya uchocheni yanaeleza kuwa, "Unaweza kukosea njia wakati wa kwenda, lakini huwezi kukosea njia wakati wa kurudi, mmeshaifahamu njia walichofanya 2019 hakitajirudia, wangapi nyumbani mna majembe, wangapi mna visu nyumbani, wangapi mna panga?
"Sasa mimi ninawaambia hivi, kama kupitia polisi kama walirudia tena katika uchaguzi ili wapitishe wanayoyataka wao haki ya Mungu safari hii majembe yatakuwa na matumizi mengine 'wakiwananihii' na nyie mnafanyaje? Mnawananihii".
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED