RAIS Samia Suluhu Hassan ameonya kwamba hataki kusikia kesi za wanafunzi wameshindwa kumaliza masomo yao kutokana na ujauzito na endapo ikitokea atawakaba walimu wao.
Alitoa angalizo hilo jana wakati akizindua Shule ya Sekondari Samia Suluhu Hassan iliyojengwa kata ya Rwinga, kijiji cha Migerege, wilayani Namtumbo, mkoani Ruvuma.
Shule hiyo ina uwezo wa kuchukua zaidi ya wanafunzi 1,000 wa kidato cha kwanza hadi cha sita. Hadi sasa wanaoendelea na masomo shuleni huko kwa kidato cha kwanza na sita ni 548.
"Nisisikie kesi kwamba wanafunzi hawa wameshindwa kumaliza masomo yao kwa sababu ya ujauzito na ikitokea nitakabana shingo na walimu kwa sababu huku msituni hakuna kwa kutokea.
"Walimu tunajua kazi tuliyowapeni. Changamoto zenu sisi kama serikali tunazifanyia kazi, tuko pamoja nanyi wala hatutawaacha," aliwaahidi.
Rais Samia aliwataka walimu kuhakikisha wanawatunza wanafunzi hao, huku akiwaeleza kwamba Mungu amewachagua kuwa nao.
"Ninaomba watunzeni wajue masomo, watunzeni kiafya, watunzeni wajitambue kwamba wao ni wanawake, wajue misingi ya mwanamke lakini pia wajue mwanamke kama mwanamke ni kiumbe kama kiumbe mwingine na mnaweza mkatimiza ndoto zao namna dhamira zao zinavyowatuma," alisema.
Rais Samia pia alisisitiza umuhimu wa elimu kwa mtoto wa kike katika kukuza maendeleo ya jamii na taifa kwa ujumla.
"Hatua hii ni sehemu ya juhudi za serikali za kuimarisha elimu na kuongeza usawa wa kijinsia nchini.
'Shule hii ni ya mchepuo wa sayansi pamoja na masomo ya sanaa kidogo, lakini imejengwa mahususi kwa masomo ya sayansi ili kumkwamua mtoto wa kike.
"Nimefurahishwa kuona nishati safi inatumika hapa shuleni, ni moja ya miradi yangu mikubwa niliyobuni mwenyewe kwa lengo la kuwasaidia wanawake wa Afrika, watumie nishati safi ya kupikia," Rais Samia alisema.
Mkuu wa Nchi alisema wameanza na taasisi za elimu na taasisi kubwa kutumia nishati hiyo ili wanafunzi watakapoona wanapikiwa chakula kupitia gesi, wakaendeleze elimu hiyo na kuitumia majumbani mwao.
"Mkoa wa Ruvuma mwaka jana pekee shule za msingi 16 na sekondari 14 zilijengwa na hadi sasa zipo jumla ya shule 860.
Kati ya hizo, shule za serikali ni 815, mmeona serikali ilivyochangamkia sekta ya elimu, lakini jumla ya shule za sekondari 247 za mkoa huu, kati ya hizo za serikali 187.
"Hii inaonesha kwamba serikali na sekta binafsi wote wamechangamkia masuala ya elimu ndani ya mkoa huu na hayo ni maendeleo makubwa, hivyo mhakikishe watoto wote wa kike na wa kiume wanapata fursa za kupata masomo yao," aliagiza.
Rais alisema serikali imeendelea kutekeleza Mpango wa Utoaji Elimu Bila Malipo na hakuna anayetozwa ada, bali wazazi wanawapelekea watoto wao fedha kwa ajili ya matumizi madogo.
Rais Samia alisema serikali imepeleka Sh. bilioni 14.5 mkoani humo kwa ajili ya mpango huo, maarufu elimu bure na kupongeza mkoa huo kwa ongezeko kubwa la wanafunzi.
Alisema kuwa mwezi Januari mwaka huu, watoto wa awali walioandikishwa mkoani humo ni 49,396, likiwa ni ongezeko la wanafunzi 7,256 kulinganishwa na mwaka jana, walikuwa 52,636 sawa na ongezeko la watoto 7,775.
Rais wa Serikali ya Wanafunzi katika shule hiyo alimshukuru Rais Samia kwa kuwajengea shule bora na kumwomba kuwapatia usafiri kwa ajili ya matumizi ya yao, ombi ambalo Rais aliridhia.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais - Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mohamed Mchengerwa, alisema shule hiyo ni miongoni mwa 26 ambazo zimejengwa katika mikoa 26 nchini na kugharimu Sh. bilioni 108.
Ni shule zilizoanzishwa kwa dhamira ya kuwakwamua watoto wa kike, mradi uliobuniwa na Rais Samia.
Waziri Mchengerwa alisema kuwa tayari wanafunzi 4,443 wamesajiliwa kusoma kwenye shule hizo nchi nzima ambao wanasoma kuanzia kidato cha kwanza.
Mbunge wa Namtumbo, Vita Kawawa, alimpongeza Rais Samia kwa kuwajengea shule hiyo mahususi kwa masomo ya sayansi ambayo itakwenda kumkomboa mtoto wa kike.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED