WIKI hii tumeshuhudia matukio mbalimbali katika soka kwa hapa nyumbani na kuwapa burudani na furaha mashabiki wa mchezo huo pendwa.
Baadhi ya matukio hayo ni pamoja na tuzo za wanamichezo bora waliofanya vizuri msimu uliopita wa 2023/2024, tukashuhudia klabu ya Yanga ikifanya vizuri kwenye tuzo hizo.
Lakini baadaye kukawa na matamasha ya klabu kubwa hapa nchini, Simba na Yanga ambayo yalipishana kwa siku moja na kuteka hisia za mashabiki wa timu hizo.
Kama hiyo haitoshi, baada ya matamasha hayo sasa ikafuatia michezo miwili ya nguvu ya nusu fainali ya Ngao ya Jamii ikiwa ni kiashirio cha kufunguliwa kwa pazia la Ligi Kuu msimu wa 2024/2025.
Michezo hiyo ni ile ya Simba dhidi ya Yanga uliochezwa kwenye uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam na ule wa Coastal Union dhidi ya Azam FC uliochezwa kwenye uwanja wa New Aman Complex, Zanzibar.
Siku moja baadae, Bodi ya Ligi Kuu ikatangaza ratiba ya msimu mpya wa Ligi wakizipanga Simba na Yanga kukutana Oktoba 19 kwenye mchezo wa mzunguko wa kwanza.
Kutokana kwa ratiba hi,i niwazi sasa tunaanza msimu mpya, msimu uliosubiriwa kwa hamu kubwa na mashabiki wa soka baada ya msimu wa 2023/2024 kumalizika Mei mwaka huu.
Hii ni ishara ya taa ya kijani kwa klabu zote zinazoshiriki Ligi Kuu msimu huu mpya kuwa sasa ziwe tayari.
Kimsingi mashabiki wa soka na wapenzi wa mchezo huo wanatarajia kuona Ligi yenye upinzani mkubwa, na yenye kuleta msisimko zaidi.
Tunavishauri vilabu vyetu vijipange na vipambane kutoa ushindani kuanzia mwanzo mpaka mwisho wa ligi na isiwe ligi ya timu mbili au tatu wakati kuna timu 16 zinazoshiriki.
Kila timu ilikuwa na muda wa kutosha wa kujiandaa kabla ya filimbi ya kuashiria kuanza msimu mpya wa Ligi, hivyo hatutarajii visingizio vyovyote kwenye kushindwa kwao.
Zipo timu zenye 'msuli mkubwa' ambazo zilienda kufanya maandalizi yao nje ya Tanzania, lakini zipo zile ambazo zilitoka mikoani mwao na kwenda mikoa mingine kuweka kambi.
Wadau wa soka tunataka kuona Ligi kweli ikipigwa, tunataka kuona kila msimu ligi inakuwa ngumu zaidi ya msimu uliopita, hii ndio itafanya soka letu lizidi kwenda mbele.
Klabu ziache zisingizio visivyo na mashiko pale wanapofanya vibaya, zijikite kwenye kutambua makosa na kuyafanyia kazi haraka ili kuendelea kufanya vizuri.
Kwa timu zilizopanda daraja nazo zitambue zinaweza kufanya vizuri kama zitapambana na kufuata misingi ya ushindani, haitapendeza kuziona zikichukua miaka mingi kupanda daraja, lakini zikatumia msimu mmoja tu kushuka daraja, waige kwa Mtibwa Sugar ambao wamekaa kwa miaka zaidi ya 23 bila kushuka daraja tangu ilipopanda kwa mara ya kwanza.
Kwa ujumla tunazitakia kila la heri timu zote kwenye msimu huu mpya ambao unaanza Ijumaa ijayo, tunatarajia ushindani mkubwa kutoka kwao, kila la heri kwa msimu mpya 2024/2025.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED