Mauaji mtoto mwenye ualbino hayavumiliki

Nipashe
Published at 01:07 PM Jun 19 2024
news
Picha: Mtandao
Mtoto aliyeuawa mwenye ualbino, Asimwe Novath.

BAADA ya mtoto mwenye ualbino kutekwa mikononi mwa mama yake na kutoonekana kwa wiki kadhaa, taarifa zimeripoti kuwa amekutwa akiwa ameshafariki na kutupwa kwenye mtaro huku baadhi ya viungo vyake vikiwa vimekatwa.

Taarifa hizo zimepokewa na wengi kwa huzuni hasa ikizingatiwa kuwa aliyedhulumiwa maisha yake ni mtoto asiye na hatia.

Uchungu anaopitia mama wa mtoto huyo hauwezi kulinganishwa na kitu chochote ni jambo ambalo hataweza kulisahau katika maisha yake yote.

Vitendo vya kutekwa na hata kuuawa kwa watu wenye ualbino vikuwa vikijitokeza nchini na kuweka jamii hiyo katika hali ya wasiwasi.

Watu wenye ualbino wana haki ya kuishi kama wengine kama Katiba ya Jamhuri ya Muungano inavyosema.

Watu hawa wanawindwa hata wanapokuwa wamelala jambo linalowanyima haki ya kuishi kama binadamu wengine.

Matukio haya yanahusishwa na imani za kishirikina na baadhi ya waganga wa jadi wanatuhumiwa kuhusika kushawishi watu kufanya matukio hayo.

Kuhusishwa kwa baadhi ya waganga wa jadi kumedaiwa kutokana na kuwadanganya wateja wao kuwa viungo vya watu wenye ualbino vikitengenezewa dawa, wanapata utajiri wa haraka haraka.

Vitendo hivi vya mauaji ya watu wenye ualbino, kukatwa viungo na kutekwa vimedaiwa vikijitokeza wakati biashara za madini zikishamiri na kila wakati inapokaribia kipindi cha uchaguzi.

Ndiyo maana kumekuwa na imani kuwa vitendo hivyo vinafanyika kwa kuamini mambo ya nguvu za giza ambazo zinawaondolea watu wasiokuwa na hatia haki ya kuishi.

Kutekwa kwa mtoto mwenye umri wa miaka miwili mwenye ualbino (sasa ni marehemu), kulizua taharuki kubwa.

Mtoto huyo aliibwa kijijini kwao Buamula, mkoani Kagera akiwa mikononi mwa mama yake na watu wasiojulikana.

Kwanini matukio kama haya yaendelee kutokea nchini kila mara, huku baadhi ya wahalifu wakikamatwa na wengine kupata adhabu kali?

Matukio haya yanasababisha watu wenye ualbino kuomba ulinzi ili wakiwa kwenye shughuli zao au wakiwa kwenye makazi yao wasiwe na wasiwasi wa kuvamiwa na kufanyiwa vitendo vibaya.

Tanzania inasifika kwa kuwa nchi yenye amani na utulivu na wananchi wake wako huru kutembea bila kuwa na wasiwasi, lakini watu wachache wenye uroho wa utajiri wanataka kuitia doa kwa vitendo vya kinyama wanavyowafanyia binadamu wenzao.

Pamoja na wanaharakati wanaopigania haki za binadamu kupiga kelele kuhusu matukio hayo na kutaka watu wenye ualbino wasichukuliwe kama viumbe tofauti, bado watu wenye imani potofu wanaendeleza vitendo hivyo.

Serikali kwa kushirikiana na vyama vya watu wenye ualbino vinatoa elimu ya kupambana na matukio hayo na kuna wakati hali hiyo ilitulia, lakini yameanza kujitokeza tena kutokana na baadhi ya watu kutaka utajiri wa haraka bila kufikiria uhai wa watu wengine.

Unapomuua binadamu mwenzako kwasababu ya kutaka mali, huo utajiri utakuwa na raha nao? Hivi wanaofanya vitendo hivyo wana hofu ya Mungu kweli? Watu wote wanapaswa kupaza sauti kukemea unyama huo.

Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kimekuwa mstari wa mbele kutetea haki za binadamu na katika tukio hili la kutekwa kwa mtoto wa miaka miwili kimetaka serikali kupitia vyombo vyake vya ulinzi, mtoto huyo apatikane.

Pia, ni muhimu kila mtu kuweka ulinzi dhidi ya mwenzake ili yanapojitokeza matukio kama hayo iwe rahisi hatua kuchukuliwa haraka.