WATANZANIA jana wameadhimisha Sikukuu ya Nanenane ambayo kila mwaka hufanyika mwezi wa nane tarehe nane.
Maadhimisho haya hukutanisha wakulima wakubwa na wadogo kutoka mikoa mbalimbali ya Tanzania ambao hubadilishana uzoefu na kupata elimu ya kilimo bora.
Sherehe hizo hutoa fursa kwa wakulima wadogo kujifunza kutoka kwa wakubwa kwa lengo la kukifanya kilimo nchini kuwa na tija, na uzalishaji bora.
Hakika sherehe hizi hubadili mandhari ya maonesho na kufanya kuonekana kuwa kijani kutokana na mazao yanayostawishwa kwa kuzingatia njia bora za kilimo.
Kilimo cha kisasa na kile cha asili kinatofauti kubwa. Mathalani, cha asili kilikuwa kikizingatia mbegu za asili ambazo pamoja na mazao yake kuwa na ladha nzuri, lakini hayatoi mazao mengi.
Kwa kilimo cha kisasa ambacho kinatumia mbegu za kisasa zinazozalishwa kisasa, zinatoa mazao mengi na kinatoa mazao mengi katika sehemu ndogo ya ardhi na kwa muda mfupi.
Kumekuwapo na masomo ya mashamba ambayo huonesha jinsi kilimo cha kisasa kinavyosaidia kuzalisha mazao mengi na kwa muda mfupi hali inayosaidia kukabiliana na tatizo la njaa.
Sikukuu ya Nanenane huonesha pia ufugaji wa kisasa kuanzia wa kuku hadi wanyama na tofauti kubwa huonekana kati ya ule wa asili na wa sasa.
Kwa ujumla, maonesho ya Nanenane hutoa fursa kubwa ya wakulima kujifunza mpaka kwenye ufugaji wa samaki ambao kwa sasa umepamba moto na kutoa matokeo bora.
Wakulima hufundishwa jinsi ya kufuga kwa kutumia eneo dogo, ambalo hutoa mazao mengi na kuleta faida kubwa kwa mfugaji.
Kuna utaalamu wa kufuga samaki kwa kutumia matangi ya maji ambayo hukatwa katikati na kuokoa mtu kutumia eneo kubwa.
Ufugaji huu pia humsaidia mtu asiyekuwa na nafasi ya kutosha kwenye eneo lake kuendelea kufaidi matunda ya ufugaji na kupata kipato kinachomwezesha kumudu maisha ya kila siku.
Kwa wakulima na wafugaji, Siku ya Nanenane ni muhimu kwao kuendelea kupata ujuzi na kubadilishana uzoefu kwa wenzao waliopiga hatua na kufikia nafasi nzuri.
Kilimo kinalipa na kinaweza kubadili maisha ya mtu bila kutegemea ajira kutoka serikalini au kwenye kampuni binafsi.
Wengi waliojaribu kilimo, wameamua kuacha ajira na kujikita kwenye sekta hiyo kwa sababu wameona manufaa yake.
Kilimo cha matunda ni kati ya kilimo kilichobadili maisha ya wakulima wengi. Mathalani, matunda aina ya parachichi yamekuwa na soko kubwa ndani na nje ya nchi na kusababisha wafanyabiashara wengi kutoka nje ya nchi kwa mfano nchi jirani ya Kenya na Afrika Kusini kuja kuyafuata matunda hayo nchini moja kwa moja.
Kilimo cha maua pia kimetoa fursa kubwa ya soko la nje ya nchi na kubadili maisha ya wakulima wengi wa kilimo hicho. Hivi sasa, maua yana soko kubwa kutokana na kutumika kwenye mapambo ya sherehe mbalimbali, kwenye upambaji wa mikutano, ofisini na kwenye misiba.
Kina mama wengi wanamiliki mashamba ya maua na kufungua kampuni zao na sasa wanaishi maisha mazuri bila kutegemea waume zao au ajira.
Pia, wamesaidia kutoa ajira kwa watu wengine kwa kuyaongezea thamani hasa kutengeneza mashada yanayotumika kupamba kwenye sherehe mbalimbali.
Kilimo na ufugaji vimebadili maisha ya wengi na sasa wanaishi bila kupata mawazo ya wapi watapata pesa.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED