MSIMU mpya wa Ligi Kuu Tanzania Bara wa mwaka 2024/2025 ulianza rasmi jana kwa mchezo mmoja uliochezwa kati ya wenyeji Pamba Jiji FC dhidi ya Maadande wa Prisons kutoka Mbeya.
Hii ni baada ya kuisubiri kwa zaidi ya miezi mitatu baada ya msimu wa 2023/2024 kumalizika.
Lakini baada ya msimu huo kumalizika, ndipo mchakato wa usajili ulianza kwa vilabu mbalimbali vinavyoshiriki Ligi Kuu na hata madaraja ya chini kuanza kusaka nyota wapya ili kuimarisha vikosi vyao.
Kwa siku za karibuni katika kipindi hicho cha dirisha la usajili kuna matukio mbalimbali yametokea yanayohusu mvutano wa usajili kuelekea msimu mpya.
Zipo timu, hususani za Ligi Kuu Tanzania Bara ambazo ziliwekewa pingamizi katika mchakato huo kwa sababu mbalimbali.
Tumesikia kilichotokea kwenye usajili wa Simba kwa wachezaji Lameck Lawi kutoka Coastal Union, Awesu Awesu aliyekuwa anaichezea KMC na Yusuph Kagoma.
Kimsingi viongozi wa klabu zetu na wachezaji wanapaswa kuheshimu mikataba wanayoingia ili kutoleta mvutano wakati upande mmoja unapotaka kuondoka au kuvunja mkataba huo.
Kwa bahati mbaya katika suala la usajili kwa miaka mingi sana tumekuwa tukifanya kiholela holela na ndiyo maana kumekuwa na kesi nyingi zinazohusu mikataba kwenye Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na lile la Kimataifa (FIFA).
Inawezekana Tanzania ikawa kinara kwa kuwa na kesi za mara kwa mara zinazohusu mikataba kule FIFA, hii haipendezi na inalitia aibu soka letu.
Ifike sehemu ‘ujanja ujanja’ uwekwe pembeni, viongozi na wachezaji wafuate taratibu kwenye kuvunja mikataba kuepuka migogoro isiyokuwa na faida kwenye soka letu.
Mchezaji anapotaka kuvunja mkataba kwenye timu moja baada ya kupata au kuahidiwa malisho mazuri kwenye timu nyingine, basi akae na uongozi wa klabu yake na wakubaliane ili aondoke kwa amani bila kuleta mvutano.
Pia kwa viongozi wa klabu, waache tamaa pale wanapoona mchezaji anakwenda kunufaika zaidi, wapo ambao wanajua kabisa kuwa mchezaji hana mkataba au umebaki chini ya miezi sita, lakini wanaweka kauzibe na hila kwenye kumruhusu mchezaji.
Hapa ndipo tunaposikia mchezaji anasema amemaliza mkataba kwenye timu yake na muda huo huo viongozi wa timu hiyo wanasema mchezaji huyo bado ana mkataba nao.
Tuache ubabaishaji kwenye masuala ya msingi, taratibu na kanuni zimewekwa ili kuepuka mvutano usiokuwa wa lazima, kila upande kwa maana ya klabu na wachezaji wanapaswa kuzifuata.
Hatutaki kurudi nyuma, tulipokuwa tunaona mchezaji akifungiwa kwa sababu ya kusaini mikataba kwenye klabu mbili kwa wakati mmoja, au klabu kutozwa faini kwa sababu ya kumsajili mchezaji mwenye mkataba na klabu nyingine, tumeshatoka huko.
Klabu kabla ya kumsajili mchezaji yeyote ijiridhishe kwanza kama kweli mchezaji huyo hana mkataba ulio hai na timu yake, hakuna sababu ya kufanya sajili za vificho, klabu zikae mezani kujadiliana, tunaamini kila timu ipo kwa ajili ya kufanya biashara kwani mpira wa sasa ni biashara.
Kwa kumalizia, kwa zile sajili ambazo Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), imezitolea maamuzi kutokana na mvutano, basi klabu husika zikae meza moja na kumalizana kwa mustakabali wa soka letu pia kwa mustakabali wa wachezaji husika ambao mpira ndio kazi yao inayowasaidia kuendesha maisha.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED