Elimu kwa umma itolewe kuhusu kufanya kazi badala ya matambiko

Nipashe
Published at 10:25 AM Aug 14 2024
treni
Picha: Mpigapicha Wetu
treni

KATIKA gazeti la Nipashe toleo la jana, kulikuwa na habari kwamba baadhi ya abiria wa treni inayopita katika Kijiji cha Katambile, Nsimbo mkoani Katavi, wanadaiwa kurusha sarafu katika Mto Ugala ulioko wilayani Nsimbo kwa imani ya kutatuliwa shida zao.

Imani kama hiyo si ngeni katika taifa la Tanzania kwa kuwa wengine wamekuwa wakienda kwenye mti mikubwa kama mibuyu kufanya matambiko na kuweka sadaka mbalimbali kama vile vyakula na fedha. Pia, wengine wamekuwa wakienda kwenye njia panda ya barabara au makutano ya njia na kuvunja nazi au kumwaga vyakula kwa imani kwamba watafanikiwa katika shida zao.  

Kwenye Kijiji cha Katyambikwe, ambacho kinamaanisha kwamba, mtu anatakiwa akafanye matambiko, ambapo watu wanadaiwa kutupa sarafu za Sh. 50, 100, 200 na 500 kwenye mto uliopo sehemu hiyo. Baadhi ya wananchi na viongozi wa eneo hilo wamehojiwa na kuthibitisha kuwa jambo hilo ni la kweli na limekuwa likifanyika kwa muda mrefu.  

Imebainishwa kwamba eneo hilo ambalo ni maarufu kwa jina la ‘Tutani”, treni inapofika mahali hapo, abiria wenye imani hiyo hurusha sarafu hizo kupitia mabehewa ya madirisha ikiwa ni njia ya kutimiza maelekezo ya waganga wao.  

Jambo hilo linafanyika katika eneo la treni itokayo Tabora kwenda Mpanda mkoani Katavi,  halina tofauti na maelekezo ya waganga hao kama ya kuweka vitu chini ya miti, kupeleka wanyama kama kuku na mbuzi kwa waganga ili kufanyiwa kafara. 

Kwa mujibu wa mkazi mmoja wa Kijiji cha Katyambikwe,  jambo hilo ni desturi kwa watu na limekuwapo enzi na enzi. Watu wanaokwenda kwa waganga wanaulizwa watapita njia gani watokapo huko na wanapo jibu watasafiri kwa treni, basi wanaelekezwa wakifika mtoni hapo, watupe sarafu za fedha za Kitanzania ili watoe sadaka huku wakiaminishwa kuwa watafanikiwa kwa kufanya hivyo. 

Baadhi ya watu wanaofanya hivyo ni wakulima ambao wakati mwingine hubeba dawa zinazodaiwa kuwa zitawasaidia katika shughuli zao, hivyo wanapofika kwenye mto huo wanatakiwa kutoa sadaka ya fedha kwa kurusha sarafu kwenye mto. Watu hao wamekuwa wakifanya hivyo kwa imani kwamba wakitumia dawa ambayo katika baadhi ya mikoa ya Nyanda za Juu Kusini huitwa ‘Ndimilo’ (dawa ya kulimia), watapata mazao mengi. 

Jambo la kujiuliza kwani ni zaidi ya miaka 60 tangu nchi ipate uhuru huku mamilioni ya watu wakiwa wamepata elimu na mafundisho ya kidini kuhusu mila potofu bado mambo kama hayo yanaendelea kutendeka. Bado wako Watanzania wanaoamini kwamba bila kufanya matambiko na kwenda kwa mganga kufanyiwa dawa hawawezi kufanikiwa. 

Viongozi mbalimbali wa serikali na wa dini wamekuwa wakisisitiza kuwa ili mtu afanikiwe ni lazima atumie juhudi na maarifa na kwamba kazi halali pekee ndiyo itakayomfanya kufikia malengo yake. Elimu hii inapaswa kuendelea kutolewa na viongozi wanapokuwa majukwaani badala ya watu kuendekeza imani na mila potofu zilizopitwa na wakati.  

Eneo la Katyambikwe linapaswa sasa kuangaliwa kwa jicho la pili kwa kuchukua hatua dhidi ya watu wanaotupa sarafu kwenye mto kwa imani za kishirikina kuwa wanapofanya hivyo watatatuliwa shida zao au kufanikiwa katika malengo yao.  

Serikali kupitia vyombo vya ulinzi na usalama, haina budi kuweka ulinzi eneo hilo kwa sababu watu hao wanavunja sheria.  Kwa mujibu wa Sheria ya Benki Kuu ya Tanzania, fedha ni tunu ya taifa na kila mmoja ana wajibu wa kuilinda na kuitunza na mtu yeyote atakayeichezea fedha atachukuliwa hatua.