Wanavyofunguka, yaliyoko mazikoni..

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 06:52 AM Apr 27 2024
Mazishi.
Picha: Mtandaoni
Mazishi.

MAKALA iliyopita kwenye safu hii iliyokuwa na kichwa cha habari, 'misiba ya sasa, ukilinganisha na zama zile, imebadilika kupitiliza, ' imeonekana kuibua wasomaji wengi sana wa gazeti hili, ambao walipiga simu na kutuma meseji zao walionekama kuguswa mno.

Baadhi walikuwa wanapongeza, lakini wapo walioongezea baadhi ya matukio ambayo wameyashuhudia wao kwenye misiba mbalimbali, inayounga mkono makala ya wiki iliyopita.

Kutokana na wingi wa wasomaji kuonekana kuguswa nimeona leo tena niirudie, lakini kwa kiasi kikubwa nitaweka kile ambacho wasomaji wenyewe wamekileta.

Kabla ya kufanya hivyo, tuweke mambo sawa ili anayesoma kwa mara ya kwanza ajue mada ilikuwa ni nini?

Kiufupi niliandika kuwa mienendo ya watu siku hizi misibani imebadilika kabisa, siyo kama ilivyokuwa zamani.

Niliandika kuwa zamani majirani wanapofika msibani kitu cha kwanza ni kumfariji mfiwa, kuchukua watoto wake wote wenye umri mdogo na kuwaondoa eneo la tukio, wakipelekwa nyumba jirani ambako watafanyiwa kila kitu, wataoga, na watachangishana pesa kuhakikisha waliofika awali kwenye msiba watakula bila wafiwa kutoa hata senti moja, lakini pia walikuwa na walinzi wa wafiwa ili wasiibiwe.

Kikubwa zaidi ni kwamba muda wote watakuwa na mfiwa, wakihakikisha halii moja kwa moja, badala yake kumbembeleza kula chakula, na mahitaji mengine muhimu ili aendelee kuwa na nguvu.

 Sehemu yenyewe ya msiba kila mmoja alikuwa na uso wa huzuni na simanzi kiasi kwamba mtu unapopita huwezi hata kuuliza kama kuna msiba au la, pia watu wanaswali, wanasali na kuimba kwa hisia kali.

Kinyume chake, mienendo ya watu misibani siku hizi inahuzunisha kuliko hata msiba wenyewe.

Watu kama wapo kwenye sherehe. Kwenye msiba wa matajiri, watu maarufu au mastaa ni kuonyesha nguo na magari ya gharama. Mtu anashuka kwenye gari na kwenda sehemu yenye msiba huku anatabasamu, anatembea kwa mbwembwe kama vile anaenda kuweka pesa benki.

Watu wanaendelea na maisha ya kawaida, wanaongea mpira, wanataniana, wanabishana, wengine wanachati na simu mwanzo, mwisho, hakuna tofauti na mtu anavyoshinda sebuleni kwake, kama vile hakuna chochote kilichotokea. Simu ziko bize kupiga picha na kuziposti kwenye akaunti zao.

Kipengele cha kulala msibani, ndiyo kimebadilika balaa. Huwezi amini, kwa sababu hizo hizo, kundi kubwa linajaa gesti za jirani, huku wengine usiku kucha kama hawako 'pub', basi kwenye mechi za Arsenal, na haishangazi simulizi za ndoa nyingi huanzia kwenye matukio hayo.

Huko uani, kinamama wanashindana nani kaja na dela la gharama, na simu ya bei mbaya, ndugu yangu kama umekuja na kitochi, utakoma, utasimangwa na kutetwa mpaka basi.

Kwa sababu nilishaandika sana wiki iliyopita, nawapa nafasi wasomaji ambao walinipigia simu na wengine kutuma meseji zao.

"Hongera kwa kuandika habari za misiba. Kweli tupu, lakini umesahau, utawakuta kinamama wako bize kupika, lakini wakati wa kupakua kabla ya wafiwa hawajapewa chakula, wameshajipakulia chakula chao cha kutosha, nyama kibao, yaani kwao 'full' sherehe, ukichanganya na umbea juu. Zile pilikapilika za kinamama msibani zifuatilie mimi nimeona misiba zaidi ya 10, shughuli ni hiyo hiyo nakwambia," aliandika msomaji mwenye simu namba 0763 246060.

"Da! Ama kweli, umefafanua tofauti ya zamani na sasa kuhusu misiba, yaani mimi nimeishia kucheka tu, hasa ulipoanza kufafanua kinachofanyika katika misiba ya sasa. Nini kifanyike kurudisha heshima na staha ya misiba jamani?" Akaandika msomaji anayetumia namba 0717    282109.

"Hujakosea ndugu, vioja vyote msibani wachotaka watu ni kuzika tu basi," aliyeandika hivyo ni msomaji mwenye namba 0757 358484.

"Misiba ya siku hizi watu wanaenda ili mradi tu waonekane na wao walikuwepo, na wala siyo kuomboleza. Ndio maana siku hizi yale matanga ya kulala siku saba hamna tena, mnazika mnaanua tanga kila mtu anatawanyika," alisema msomaji mmoja aliyepiga simu.

"Akina mama ndiyo wanatumia huo muda kuoneshana madera ya gharama, magari, dhahabu na simu. Ole wako usiwe na 'smart phone', utachambwa balaa," mama mmoja alichangia kwa kupiga simu.

"Sasa kuna wale wanaoiga uzungu, kafiwa na mtu wake wa karibu kabisa lakini anathubutu kujiremba, wengine hadi saluni wanaenda! Wengine wavaa nguo, viatu vya bei mbaya na miwani myeusi juu, ubishoo umewajaa, hawalii machozi na kugaragara, wanaona poda au 'enjoy face', itatoka," alisema mwingine.

"Yaani marehemu anaingizwa kaburini, watu simu zao ziko bize, badala ya kuzima, kila mmoja anakwenda kupokea pembeni, tena badala ya kusema wapo msibani, kila mmoja anazungumza bila kujali." Msomaji mmoja alibainisha.

 "Siku hizi utakuta msibani baadhi ya wanawake hata kanga havai, eti anavaa suruali,  kichwa wazi  jamani! Sijui kwa nini?" Ni simu za baadhi ya wasomaji wetu.

"Maigizo yamechukua nafasi bila kusahau wanja na lipstick, kuonyeshana mitindo ya nywele na nguo, huku hisia kiduchu. Hisia zilikuwa zamani jama."

Yupo aliyepiga simu na kuongea kwa hisia sana. "Mkuu, misiba ya sasa imekua majanga sana, yaani badala ya watu kwenda msibani kusitiri na kuwafariji wafiwa badala yake misiba imegeuka vijiwe vya majungu na kuwajadili wafiwa.

Sasa mimi najiuliza kuna manufaa gani kuwajadili wafiwa tena? Zamani misibani watu walikua na heshima sana tofauti na sasa, sijui tunakwama wapi?

Mkuu niombe tuweni mabalozi wa kuikemea tabia hii tuwapo misibani kwa sababu haipendezi kabisa."

Mtu wa mwisho aliyefunga kazi alinipigia simu na kuongea maneno ambayo nayawasilisha hapa.

"Kuna siku ilitokea misiba miwili kijijini kwetu na wote walizikwa siku moja. Kaya moja ilikuwa masikini na nyingine wana kiuwezo uwezo. Yaani  watu walienda kuzika kule kwa masikini chapuchapu, wakaondoka hata bila kumaliza taratibu za kimila, wakawahi kule ambako kulikuwa na vyakula vya kutosha na pombe. Chakusikitisha waliisimanga sana ile familia masikini, jambo hili liliniuma sana. Misiba imegeuka kuwa sehemu ya maonyesho, na watu wanakuja kula na kunywa. Yaani ukifiwa kama huna milioni kama tano hivi kazi unayo. Utachekwa mpaka ukome.  Yaani wanacheka mpaka aina ya jeneza.

 Tuma meseji 0716 350534