Bodi ya Mikopo kupewa ‘meno’ zaidi

By Augusta Njoji , Nipashe
Published at 02:43 PM May 08 2024
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa mwaka huo, Waziri Prof. Adolf Mkenda
Picha: Ibrahim Joseph
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa mwaka huo, Waziri Prof. Adolf Mkenda

SERIKALI imesema kwa mwaka 2024/25 itafanya marekebisho ya Sheria ya Bodi ya Mikopo ili kuongeza ufanisi wake ikiwamo kurahisisha ufunguaji wa mashauri na utekelezaji wake.

Akiwasilisha bungeni makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa mwaka huo, Waziri Prof. Adolf Mkenda amesema wataendelea kukusanya madeni ya mikopo iliyoiva ya kiasi cha Sh. bilioni 198 kutoka sekta  ya umma na kuimarisha makusanyo kutoka sekta binafsi na isiyo rasmi.

Aidha, amesema itatafuta wanufaika wapya 40,000 wenye marejesho ya   mikopo iliyoiva ikijumuisha wanufaika wapya 5,000 wenye mikopo chechefu kutoka sekta binafsi na isiyo rasmi.

Pia amesema ufadhili kwa ajili ya shahada za juu ikiwamo eneo la fani ya mionzi na nyuklia utaanza kutolewa na itafanya tathmini ya programu 300 za masomo  mbalimbali katika vyuo vikuu nchini.

MIKOPO DIPLOMA

Pia amesema serikali itatoa mikopo kwa wanafunzi wa stashahada takribani 10,000 katika fani za kipaumbele na zenye uhaba wa wataalam nchini, zikiwamo  za sayansi na ufundi.

Amesema ili kuimarisha ushirikiano na mataifa mengine na kuongeza fursa za elimu nchini, serikali itatoa ufadhili kwa wanafunzi watano kutoka China wanaosoma lugha ya Kiswahili katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam;

Pia itatoa ufadhili kwa wanafunzi watano raia wa Oman na wanafunzi watano raia wa Hungary kusoma katika vyuo vikuu nchini kulingana na mikataba na itashiriki katika mikutano ya ushirikiano wa kikanda na kimataifa.

Amesema serikali itaandaa Mpango Kabambe wa Taifa wa Sayansi, Teknolojia na Ubunifu na kwamba itafanya utafiti wa kimkakati wa ulinganishaji katika nchi ambazo vyuo vikuu vina uzoefu wa kutumia teknolojia ya kidijiti katika ufundishaji na ujifunzaji na huduma za utawala.

Katika kuimarisha matumizi salama ya mionzi ya nyuklia nchini, Prof. Mkende amesema serikali kupitia Tume ya Nguvu za Atomiki itaendelea kudhibiti matumizi ya mionzi nchini kwa kukagua vituo 900 ikiwamo hospitali, vituo vya afya, migodi, viwanja vya  ndege, na viwanda na majengo yenye mashine za kupima mionzi ili kuhakikisha uwepo wa mazingira salama kwa wagonjwa, wafanyakazi na umma kwa ujumla.